MAN UTD-DAVID MOYES

Moyes: Mashabiki wana haki zote za kuwa na hasira na kiwango cha timu yao

Kocha mkuu wa Manchester United aliyetimu liwa David Moyes
Kocha mkuu wa Manchester United aliyetimu liwa David Moyes Reuters

Aliyekuwa Kocha mkuu wa klabu ya Manchester United, David Moyes amewashukuru mashabiki na uongozi wa timu hiyo kwa kumuamini na kumpa jukumu la kuiongoza timu hiyo katika ligi kuu ya Uingereza.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza kwa mara ya kwanza hapo jana jioni toka avuliwe madaraka yake, Kocha David Moyes amesema kuwa licha ya kandarasi yake kusitishwa lakini anashukuru kwa kupata ushirikiano mkubwa toka kwa mashabiki na uongozi wa klabu hiyo.

Moyes pia amemshukuru aliyekuwa kocha wa timu hiyo Sir Alex Ferguson kwa kumuamini na kumchagua kama chaguo sahihi kwa timu hiyo katika kuivusha kwenye kipindi kigumu ambacho timu hiyo ilikuwa nayo.

Lakini kuondolewa kwake kwenye klabu ya Manchester City kumeibua utata kwa Chama cha makocha nchini Uingereza ambacho kinadai kuwa kufutwa kazi kwa David Moyes hakukuzingatia haki wala maadili ya kazi.

Chama hicho kinasema kuwa kilichofanywa na Man utd ni kumfungashia virago na kutangaza kusitisha kandarasi ya kocha huyo hata bila ya kuwa na mazungumzo nae ya awali kabla ya kutangaza kuachana nae.

Klabu ya Manchester United Jumatatu ya wiki hii ilitangaza kuachana na kocha huyo kwa kile kinachoelezwa ni kushindwa kuingoza timu hiyo kupata mafanikio ambayo mashabiki na uongozi wa timu ulitarajia.

Moyes mwenyewe amekiri kuwa kibarua cha kuinoa timu hiyo ni kigumu na kwamba licha ya vikwazo na ugumu wa kazi aliyokuwa nayo bado hakuwahi kukata tamaa hata siku moja kuhakikisha kuwa anajaribu kuifikisha mahali fulani timu hiyo.

Katika hatua nyingine, Kocha wa muda wa timu hiyo, mkongwe Ryan Giggs tayari ameanza jukumu lake jipya kwenye timu ya kwanza ambapo atasaidiwa na mchezaji wa zamani pia wa timu hiyo Nick Butt ambao kwa pamoja wamepewa nguvu na wachezaji wakongwe wa timu hiyo kama Paul Scholes na Philip Neville.

Kibarua cha kwanza cha Ryan Giggs kitakuwa nyumbani wakati timu yake itakapoikaribisha klabu ya Norwich City.

Katika hatua nyingine taarifa zinasema kuwa, kocha wa zamani wa timu hiyo ambaye pia ni mmoja wa viongozi wa bodi ya Manchester United Sir Alex Ferguson atahusishwa kwa sehemu kubwa katika kusaka mrithi wa kudumu wa kuinoa klabu hiyo.