LIGI KUU YA UINGEREZA

Liverpool, Chelsea na Manchester City zakabana koo kuwania taji la ligi kuu ya Uingereza 2014/2015

Kocha wa Chelsea, Josee Mourinho akishangilia baada ya timu yake kupata ushindi dhidi ya Liverpool
Kocha wa Chelsea, Josee Mourinho akishangilia baada ya timu yake kupata ushindi dhidi ya Liverpool chelseafc.com

Ligi kuu nchini Uingereza imefikia hatua ngumu ya kutabiri kuwa ni nani ataibuka mshindi wa taji la mwaka 2014/2015 kati ya vinara watatu walioko kwenye kilele cha msimamo wa ligi kuu nchini humo, vinara hao, ni klabu ya Liverpool, Chelsea na Manchester City.

Matangazo ya kibiashara

Ligi hiyo imeshuhudiwa ikichukua muelekeo mwingine mara baada ya mechi za mwishoni mwa juma ambapo klabu ya Chelsea mara baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya hasimu wake klabu ya Liverpool imeipunguza kasi timu hiyo.

Kocha wa Real Madrid Josee Mourinho
Kocha wa Real Madrid Josee Mourinho Reuters

Katika mchezo uliopigwa siku ya Jumapili, klabu ya Liverpool ilihitaji ushindi ama sara ya aina yoyote dhidi ya Chelsea inayoongozwa na kocha Josee Mourinho ili ijihakikishie nafasi nzuri zaidi ya kutwaa taji hili lakini mambo hayakuwa hivyo.

Kwenye mchezo huo vijana wa Josee Mourinho walifanya kile ambacho mashabiki wa soka hawakukitarajia baada ya kufanikiwa kuchomoza na ushindi muhimu wa mabao 2-0 dhidi ya Liverpool.

Uzembe wa mabeki wa Liverpool ulitosha kumfanya mshambuliaji, Demba Ba na kiungo William kutumia nafasi hizo kupachika mabao muhimu ambayo yameshuhudia timu yao ikibakisha alama mbili tu nyuma ya vinara hao wa ligi Liverpool.

Mshambuliaji wa Liverpool, Luis Suarez
Mshambuliaji wa Liverpool, Luis Suarez REUTERS

Kwenye mechi nyingine ambayo matokeo yake yalikuwa yanasubiriwa kwa hamu kubwa ni matokeo ya mechi kati ya Manchester City na Crystal Palace mchezo ambao umeshuhudia Man City wakipata ushindi muhimu wa mabao 2-0.

Kwa matokeo haya sasa, Liverpool bado inasalia kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Uingereza ikiwa na alama 80, ikifuatiwa kwa ukaribu na Chelsea yenye alama 78, wakati Manchester City wao wanafuatia wakiwa na alama 77 huku ikiwa bado na mchezo mmoja wa ziada dhidi ya wenzake.

Iwapo Manchester City atafanikiwa kushinda mechi zake zote nne zilizobakia basi kuna uwezekano mkubwa kuwa ndiye atakayetwaa taji la mwaka huu, huku ikiziacha Chelsea na Liverpool ambazo zimesalia na mechi mbili kumaliza msimu.

Kocha wa Manchester City, Manuel Pellegrini
Kocha wa Manchester City, Manuel Pellegrini REUTERS/Stefan Wermuth

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa taji la msimu huu ni kati ya vinara hawa watatu ambapo kila mmoja anayo nafasi ya kuchukua kombe hili ambalo msimu uliopita lilitwaliwa na Manchester United ambayo iko kwenye nafasi ya saba msimu huu.

Leo usiku timu inayowania kusalia kwenye nafasi ya nne, Klabu ya Arsenal itakuwa na kibarua dhidi ya Newcastle United mchezo unaotarajiwa kuwa mgumu kwa pande zote mbili ambazo zinahitaji ushindi, iwapo Arsenal itashinda itakuwa imejiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kushika nafasi ya nne mbele ya Everton inayofukuzia nafasi hiyo.