UEFA

Atletico Madrid kumenyana na Real Madrid katika fainali ya UEFA

Wachezaji wa Atletico Madrid wakishangilia baada ya kuifunga Chelsea
Wachezaji wa Atletico Madrid wakishangilia baada ya kuifunga Chelsea REUTERS/Sergio Perez

Klabu ya soka ya Atletico Madrid ya Uhispani imefuzu fainali ya kuwania taji la  klabu bingwa barani Ulaya baada ya kuifunga Cheslea ya Uingereza mabao 3 kwa 1 katika mchuano wa marudiano wa nusu fainali uliochezwa Jumatano usiku.

Matangazo ya kibiashara

Atletico Madrid sasa itamenya na ndugu zao  Real Madrid wote wanaotokea  katika mji mmoja wa Madrid nchini Uhispania, katika fainali itakayopigwa tarehe 24 mwezi huu mjini Lisbon nchini Ureno.

Katika Histori ya UEFA ndio mara ya kwanza kwa vlabu kutoka mji mmoja kucheza katika fainali ya taji hili barani Ulaya.

Chelsea ndio iliyoanza kupata bao kupitia mshambulizi Fenardo Toress ambaye zamani alikuwa anaichezea Atletico Madrid katika dakika ya 36 ya mchuano huo.

Dakika nane baadaye, Adrian Lopez aliisawazishia Atletico Madrid, na baadaye Diego Costa akafunga bao la pili kupitia mkwaju wa penalti kabla ya Arda Turan kufunga la tatu dakika 18 kabla ya kumalizika kwa mchuano huo.

Mara ya mwisho kwa Atletico Madrid kufuzu katika fainali ya michuano hii ya UEFA ilikuwa takribani miaka 40 iliyopita na ni mara ya kwanza watakutana na wapinzani wao Real Madrid katika hatua ya fainali .

Itakuwa mara ya 17 kwa vlabu viwili kutoka nchi moja kukutana katika fainali ya UEFA, mara ya mwisho kwa vlabu vya Uhispania kukutana katika fainli kama hii ilikuwa ni mwaka 1999 ambapo Real Madrid waliwafunga Valencia mabao 3 kwa 0.

Kocha wa Chelsea Jose Mourihno amepoteza michuano minne iliyopita ya nusu fainali akiwa kocha wa klabu ya Real Madrid na ndoto yake ya kuwa kocha wa kwanza duniani kunyakua taji la UEFA na vlabu vitatu tofauti imegonga mwamba.

Wachambuzi wa soka wanasema mabeki wa Chelsea walidhoofika na wamemwangusha Mourihno.

Siku ya Jumanne, Real Madrid ilifuzu baada ya kuishangaza bingwa mtetezi Bayern Munich ya Ujerumani kwa mabao 4 kwa 0 na kwa ujumla kufuzu kwa ushindi wa mabao 5 kwa 0 kutokana na ushindi wa nyumbani wa bao 1 kwa 0.