ITALIAN OPEN

Novak Djokovic amshinda Rafael Nadal na kutwaa taji la Italian Open

Novak Djokovic akionesha kombe alilotwaa kwenye michuano ya Italian Open Jumapili tarehe 18.05.2014.
Novak Djokovic akionesha kombe alilotwaa kwenye michuano ya Italian Open Jumapili tarehe 18.05.2014. eurosport.com

Mchezaji tennesi Novak Djokovic amefanikiwa kushinda taji lake la tatu la michuano ya Italian Open na kuweka matumaini ya kutwaa taji la french open baada ya kumfunga mhispania Rafael Nadal kwenye fainali ya Rome.

Matangazo ya kibiashara

Novak Djokovic amefanikiwa kumshinda bingwa mtetezi wa michuano hiyo Rafael Nadal kwa seti mbili kwa moja kwa matokeo ya 4-6, 6-3 na 6-3 katika mchezo uliodumu kwa saa mbili na dakika 19.

Kwa ushindi wa hapo jana, Djokovic amefanikiwa kujiwekea rekodi binafsi ya kumfunga kwa mara tatu mfululizo Nadal katika michuano mitano tofauti ya ATP Masters katika matukio 1000.

Kwa ushindi huu dhidi ya Nadal, Djokovic sasa anajiandaa kushiriki michuano ya French Open inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa juma hili ambapo Nadal ndiye bingwa mtetezi mwenye historia ya kutwaa taji hilo mara 8.

Wachambuzi wa mchezo huu wanadai kuwa licha ya rekodi nzuri aliyonayo Nadal kwenye michuano ya French open na ushindi katika hatua ya nusu fainali dhidi ya Djokovich mwaka jana, bado hawaoni kama Nadal ananafasi ya kutetea taji hilo.

Hii ni mara ya kwanza kwa Nadal kupoteza michezo miwili kwenye uwanja wa usiokuwa na nyasi toka mwaka 2004 alipofungwa kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya Monte Carlo na Barcelona.

Akizungumza punde baada ya kupoteza mchezo huo, Nadal amesema kuwa mchezo ulikuwa mgumu sana kwake na kwamba kwenye mashindano haya alicheza mechi tatu ngumu ambazo zilimfanya achoke na akakutana na mmoja kati ya wachezaji bora duniani wa Tennesi.

Kwa upande wake, Djokovic, amesema kuwa ushindi huu umekuja wakati wa huzuni kufuatia nchi yake ya Serbia juma lililopita kukumbwa na na mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu 35 na kusababisha wengine maelfu kupoteza makazi yao.