SOKA

Kombe la dunia: Wachezaji wa Cameroon kulipwa Dola 104,000 kila mmoja

Mshambulizi wa Cameroon Samuel Eto'o
Mshambulizi wa Cameroon Samuel Eto'o

Shirikisho la soka nchini Cameroon na serikali zimekubaliana kwa pamoja kumlipa kila mchezaji Dola laki moja na elfu nne wakati wa michuano ya kombe la dunia nchini Brazil mwezi ujao.

Matangazo ya kibiashara

Fedha hizo zitalipwa kwa wachezaji wa kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 wakati wa michuano hiyo.

Hili suala la mshahara kwa wachezaji wa Cameroon limekuwa tata katika siku za hivi karibuni na hatua hii inaangiziwa kuwa litasaidia kumaliza mzozo huu ambao umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu.

Kikosi hicho kikiongozwa na nahodha Samuel Eto'o kilikuwa kimetishia kugoma kuanzia siku ya Ijumaa ikiwa marupurupu yao yangewekwa wazi na shirikisho hilo la soka.

Mashabiki wa soka nchini humo wamekuwa wakishinikiza kikosi cha Cameroon kuiletea sifa nchi hiyo katika michuano ya Kimataifa kama ilivyokuwa miaka ya 80 na 90 wakati wachezaji kama Roger Milla wakicheza.

Mwaka 2010 Cameroon ilikuwa nchi ya kwanza kubanduliwa nje ya michuano ya kombe la dunia iliyofanyika nchini Afrika Kusini.

Siku ya Alhamisi, Cameroon inashuka dimbani kumenyana na Paraguay katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki.

Super Eagles ya Nigeria nayo ilitoka sare ya mabao 2 kwa 2 na Scotland katika mchuano mwingine wa kirafiki Jumatano usiku kwa maandalizi ya michuano hii.

Kocha Stephen Keshi hakuwatumia wachezaji wakongwe kama kipa Vincent Enyeama na kiungo wa kati John Obi Mikel katika mchuano huo wa kirafiki.

Nigeria pia itacheza na Ugiriki na Marekani katika michuano mingine ya kirafiki kabla ya kumenyana na Iran tarehe 16 mwezi ujao katika mchuano wa kwanza wa kombe la dunia katika uwanja wa Curitiba.

Mbali na hilo, zikiwa zinasalia wiki mbili kabla ya kuanza kwa michuano ya soka ya kombe la dunia nchini Brazil.

Katibu Mkuu wa shirikisho la soka duniani FIFA Jerome Valcke amesema amesikitishwa na maandalizi ya michuano hiyo hasa kutomalizika kwa uwanja wa Dunas katika eneo la Natal Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo ambao viti vya jukwaa la watu washuhuri havijawekwa vizuri.

Uwanja huo utatumika katika mchuano wa ufunguzi kati ya Mexico na Cameroon tarehe 13 mwezi ujao.