USAJILI ULAYA

Rickie Lambert ajiunga rasmi na klabu ya Liverpool kwa dau la pauni milioni 4

Mshambuliaji wa Southampton, Rickie Lambert ambaye sasa anajiunga na klabu ya Liverpool
Mshambuliaji wa Southampton, Rickie Lambert ambaye sasa anajiunga na klabu ya Liverpool southamptonfc

Hatimaye mshambuliaji mkongwe wa klabu ya Southamton na timu ya taifa ya Uingereza, Rickie Lambert amekamilisha rasmi usajili wake wa kujiunga na klabu ya Liverpool kwa dau la paundi za Uingereza milioni 4. 

Matangazo ya kibiashara

Lambert mwenye umri wa miaka 32 hivi sasa ni miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza kilichotangazwa na kocha Roy Hodgson kuelekea kule nchini Brazili kwa michuano ya kombe la dunia mwaka huu.

Lambart ambaye wakati fulani aliitumikia Liverpool akiwa na timu ya vijana kwa miaka mitano, amesaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo kwa miaka miwili baada ya mwishoni mwa juma kufuzu vipimo vya afya.

Akizungumza na wanahabari punde baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, Lambert amesema "Siamini mpaka sasa, niliipenda sana timu hii maisha yangu yote, niliondoka nikiwa na miaka 17 na toka wakati huo sikuacha kuipenda timu hii". Alisema Lambert.

Mshambuliaji huyu akaongeza kuwa "Mara zote nimekuwa na ndoto za kucheza katika timu hii, na wakati fulani nilifikiri ndoto zakuchezea timu hii hazitatimia, na sikudhani kama nafasi hii ingetokea". Aliongeza Rickie Lambert.

Lambert hakusita kuonesha wazazi wake walivyopokea taarifa za yeye kujiunga na timu yake ya zamani, na Lambert anasema mama yake aliangua kilio cha furaha baaa ya kumpa taarifa kuwa amefanikiwa kufuzu vipimo vya afya na sasa atajiunga na vijogoo vya jiji.

Lambert amefunga mabao mawili akiwa na timu yake ya taifa, lakini amefunga magoli kumi na nne katika mechi 39 alizoitumikia klabu yake ya Southampton ambayo sasa anaicha.