UEFA-QATAR

Platin: Ntaunga mkono kupigwa kwa kura upya iwapo tuhuma dhidi ya Qatar zitathibitishwa

Michel Platin hapa akiwa mjini Doha, Qatar mwaka 2011
Michel Platin hapa akiwa mjini Doha, Qatar mwaka 2011 AFP PHOTO / KARIM JAAFAR

Rais wa shirikisho la mpira barani Ulaya, Michel Platin ametaka kuitishwa upya kwa kura ya kuamua nchi mwandaaji wa michuano ya kombe la dunia mwaka 2022, kauli anayoitoa baada ya kuibuka tuhuma kuwa nchi ya Qatar ilitoa rushwa ili kupewa nafasi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Platin amesema kuwa ataunga mkono hatua ya kufanyika kwa kura mpya ya kuamua nchi itakayoandaa fainali za mwaka 2022 iwapo tu tuhuma dhidi ya nchi ya Qatar zitathibitika kuwa ni kweli.

Kamati iliyofanikisha nchi ya Qatar inapewa nafasi ya kuandaa fainali za kombe la dunia mwaka 2022 imejikuta kwenye shinikizo kubwa baada ya gazeti la Sunday Times kuchapisha habari inayowatuhumu baadhi ya vigogo wa fifa kupewa rushwa na nchi hiyo ili kuipendelea Qatar.

Nchi ya Qatar yenyewe imekanusha taarifa hizi kwa kile inachosisitiza kuwa ushindi wa nafasi ya kuandaa fainali za mwaka 2022 ulikuwa ni ushindi halali na hakukuwa na hongo.

Michel Platini (katikati) anahusishwa na kashfa ya rushwa na nchi ya Qatar kupewa uenyeji wa fainali za fifa mwaka 2022
Michel Platini (katikati) anahusishwa na kashfa ya rushwa na nchi ya Qatar kupewa uenyeji wa fainali za fifa mwaka 2022 AFP PHOTO / FRANCK FIFE

Rais huyu wa shirikisho la mpira Ulaya amekiri kuipigia kura nchi ya Qatar kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2022 lakini akakanusha kuwa alipokea mlungula ili aipigie kura nchi hiyo.

Lakini Platin anasema kuwa iwapo tuhuma hizi zitathibitishwa basi atakuwa hana budi bali ni kupiga upya kura hiyo na kwamba nchi ya Qatar itabidi iwekewe vikwazo katika soka.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi wake wa kuipigia kura nchi ya Qatar kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2022, Platin anasema "Sijutii chochote, nadhani ulikuwa ni uamuzi sahihi kwa fifa na wapenzi wa mpira wa miguu duniani'. Alisema Michel Platin.

Mchezaji huyu wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa na ambaye amekuwa rais wa UEFA toka mwaka 2007 amesema kuwa ataamua iwapo awanie nafasi ya urais wa shirikisho la mpira wa miguu duniani fifa au la, baada ya fainali za mwaka huu kule nchini Brazil kumalizika.

Rais wa sasa wa fifa Sepp Blatter mwenye umri wa miaka 78, ameongoza shirikisho hilo toka mwaka 1998 na tayari ameonesha nia ya kutaka kutetea nafasi yake kwa mara nyingine.