BRAZIL 2014

Brazil 2014: Cote Dvoire yabanduliwa na Ugiriki kwa huzuni

Bao la Penalti la Georgios Samaras dhidi ya Cote Dvoire
Bao la Penalti la Georgios Samaras dhidi ya Cote Dvoire REUTERS/Eddie Keogh

Timu ya taifa ya Cote Dvoire imekuwa timu ya pili ya Afrika kubanduliwa nje ya michuano ya soka ya kombe la dunia baada ya kufungwa na Ugiriki mabao 2 kwa 1 katika mchuano wa kutamatisha kundi la C Jumanne usiku.

Matangazo ya kibiashara

Hadi dakika za nyongeza za mchuano huo, Cote Dvoire walikuwa na matumaini ya kufika katika hatua ya 16 bora kabla ya Ugiriki kupewa penalti ya kutatanisha na baadaye kufungwa na mshambulizi wa Celtic Georgios Samaras.

Ugiriki ndio iliyoanza kupata bao baada ya Andreas Samaris kufunga katika dakika 42 ya mchuano huo kabla ya muda wa mapumziko baada ya makosa ya beki wa Cote Dvoire Cheick Tiote kutoa pasi mfupi iliyompata mchezaji wa Ugiriki.

Hata hivyo, dakika 74 kipindi cha pili mshambulizi Wilfried Bony aliisawazishia Cote Dvoire baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Gervinho.

Mshambulizi wa Cote Dvoire Didier Drogba akimchenga mchezaji wa Ugiriki
Mshambulizi wa Cote Dvoire Didier Drogba akimchenga mchezaji wa Ugiriki REUTERS/Mike Blake

Muda mfupi baada ya kukamilika kwa mchuano huo, Kocha wa Cote Dvoire Sabri Lamouchi alitangaza kujiuzulu.

“Mkataba wangu unakamilika na michuano hii ya kombe la dunia, hatukufanya vizuri katika michuano ya kombe ya mataifa bingwa barani Afrika na sasa michuano hii,” Lamouchi alisema.

“Cote Dvoire ni taifa kubwa katika mchezo wa soka. Mchuano huu tumeonewa.Baada ya kila mtu kutia bidii na kujitoa sisi wote tumehuzunishwa sana,” aliongezea.

Mfaransa huyo alijiunga na Cote Dvoire mwaka 2012 kuiongoza katika michuano ya kombe la mataifa bingwa barani Afrika na pia michuano ya kufuzu kwa kombe la dunia na hatimaye michuano hii ya kombe la dunia nchini Brazil.

Matokeo ya Cote Dvoire yamewahuzunisha mashabiki na wapenzi wa soka barani Afrika, hasa wakikumbuka penalti ya kutatanisha waliyopewa Ugiriki, na wawakilishi hao wa Afrika wanaondolewa katika michuano mitatu ya kombe la dunia iliyopita.

Mashabiki wa cote Dvoire jijini Abidjan
Mashabiki wa cote Dvoire jijini Abidjan REUTERS/Luc Gnago

Naye kocha wa Ugiriki Fernando Santos alisema “ Kwa wapenzi wa soka nchini Ugiriki nendani mitaani na mshereheke.,”

Nahodha wa Ugiriki Giorgos Karagounis naye alisema “ Tulikuja kufika katika hatua ya mwondoano, hatujawahi kufika hapo, na tumefanikiwa kwa njia ya kipekee.,”

Ugiriki sasa itamenyana na Costa Rica katika hatua ya mwondoano siku ya Jumapili.

Andreas Samaris wa Ugiriki akipambana na Kolou Toure wa Cote Dvoire
Andreas Samaris wa Ugiriki akipambana na Kolou Toure wa Cote Dvoire REUTERS/Mike Blake

Katika matokeo mengine siku ya Jumanne usiku, Colombia ambao tayari wamefuzu katika hatua ya 16 bora waliwafunga Japan mabao 4 kwa 1, huku Costa Rica wakitoka sare ya kutofungana na Uingereza.

Italia nao walibanduliwa nje ya michuano hii baada ya kuwafunga Uruguay bao 1 kwa 0 na baada ya mchuano huo kocha wa Italia Cesare Prandelli alisema anajiuzulu.

Kitakachokumbukwa zaidi katika mchuano huo ni wakati mshambulizi wa Uruaguy Luis Suarez alipom'ngata beki wa Italia Giorgio Chiellini.

Kiungo wa Kati wa Italia, Claudio Marchisio naye alioneshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya mchezaji wa Uruaguy Egidio Arevalo.

Uruguay sasa watamenyana na Colombia katika hatua ya mwondoano siku ya Jumamosi.

Siku ya Jumatano, Nigeria watapambana na Argetina, Iran na Bosnia and Herzegovina.

Mechi nyingine, Ecuador na Ufaransa , Honduras na Uswizi.

Nigeria wanahitaji kuifunga Argetina kujihakikisha matumai ya kusonga mbele kwa sababu wana alama 4 na ni wa pili katika kundi lao, au wakitoka sare au kufungwa, waombe kuwa Bosnia and Hergovina iwafunge Iran ambao wapo katika nafasi ya tatu kwa alama 1.

Kipa wa Nigeria Vincent Enyeama
Kipa wa Nigeria Vincent Enyeama REUTERS/Suhaib Salem

Ufaransa tayari imefuzu lakini mchuano wa Jumatano utakuwa ni wa kutafuta ushindi wa kundi lao kwa sababu hadi sasa wanaongoza kwa alama sita.

Uswizi wanahitaji kuifunga Honduras ili kusonga mbele au wakitoka sare, Ufaransa wawafunge Ecuador.

Ikiwa Uswizi na Ecuador zitashinda, basi mabao yatahesabiwa ili kuamua ni nani ataingia katika hatua ya mwondoano kwa sababu timu zote mbili zina alama 3.