BRAZIL 2014

Algeria yashangilia kufuzu hatua ya 16 bora, Ghana warudi nyumbani

Maelfu ya raia wa Algeria bado wanasherehekea kufuzu kwa timu yao ya taifa alimaarufu kama  “The Desert foxes” katika hatua ya 16 bora katika michuano ya soka ya kombe la dunia inayoendelea nchini Brazil.

Islam Slimani akiishawazishia timu yake ya Algeria
Islam Slimani akiishawazishia timu yake ya Algeria Reuters
Matangazo ya kibiashara

Algeria walifuzu baada ya kutoka sare ya bao 1 kwa 1 na Urusi Alhamisi usiku katika mchuano wa kutamatisha kundi lao.

Mashabiki wa Algeria wakisherekea baada ya timu yao kufuzu
Mashabiki wa Algeria wakisherekea baada ya timu yao kufuzu REUTERS/Louafi Larbi

Urusi ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao katika kipindi cha kwanza cha mchuano huo, kabla ya Algeria kusawazisha kupitia  Islam Slimani katika kipindi cha pili cha mchuano huo.

Algeria itamenyana na Ujerumani katika hatua ya mwondoano siku ya Jumatatu juma lijalo.

Kufuzu kwa Algeria kumewakumbusha wengi mwaka 1982 ambapo Ujerumani Magharibi ilitoka sare makusudi na Austria na kuwanyima nafasi Algeria kufuzu katika hatua ya 16 bora.

Jijini Paris, polisi wanasema wamewakamata zaidi ya raia 70 wa Algeria ambao walikuwa wanafanya fujo na kuiba bidhaa baada ya Algeria kufuzu.

Mshambulizi wa Algeria Madjid Bougherra
Mshambulizi wa Algeria Madjid Bougherra www.telegraph.co.uk

Wawakilishi wengine wa Afrika Ghana, walibanduliwa nje ya michuano hiyo baada ya kushindwa kupata ushindi dhidi ya Ureno ambao waliwafunga mabao 2 kwa 1.

Kipa wa Ghana Dauda akijaribu kuokoa goli dhidi ya Ureno, Beki Yobe na Ronaldo
Kipa wa Ghana Dauda akijaribu kuokoa goli dhidi ya Ureno, Beki Yobe na Ronaldo

Licha ya Ureno kupata ushindi huo, haikufuzu kwa sababu ilifanya vibaya katika michuano yake  miwili ya ufunguzi.

Mshambulizi wa Ureno Cristiano Ronaldo akimchenga mchezaji wa Ghana
Mshambulizi wa Ureno Cristiano Ronaldo akimchenga mchezaji wa Ghana REUTERS/Jorge Silva

Mataifa ya Ujerumani na Marekani yamefuzu licha ya Marekani kufungwa na Ujerumani bao 1 kwa 0.

Hii ndio mara ya kwanza tangu kuanza kwa michuano ya soka ya kombe la dunia mwaka 1930 kwa timu mbili za Afrika kufuzu katika hatua ya mwondoano.

Asamoh Gyan wa Ghana licha ya timu yake kuondolewa katika michuano hiyo, anaweka Historia kuwa mchezaji wa kwanza wa Afrika kufunga mabao 6 katika kombe la dunia na kuvunja rekodi ya Roger Milla kutoka Cameroon aliyefunga mabao 5 miaka ya tisini.

Asamoah Gyan mchezaji wa Ghana
Asamoah Gyan mchezaji wa Ghana REUTERS/Jorge Silva

Nacho kikosi cha Nigeria hakijahudhuria mazoezi siku ya Ijumaa kwa madai kuwa wachezaji hawajalipwa marupurupu yao.

Wachezaji wa Super Eagles wanadai marupurupu yao baada ya kufika katika hatua ya 16 bora.

Kikosi cha Super Eagles chini ya kocha Stephen Keshi walistahili kufanya mazoezi katika mji wa Campinas lakini hawakusafiri kwa sababu walikuwa kikaoni kujadili suala hilo.

Nigeria wanajiandaa kumenyana na Ufaransa katika hatua ya mwondoano siku ya Jumatatu juma lijalo, baada ya kumaliza wa pili katika kundi lao kwa alama 4.

Shola Ameobi na Vincent Enyeama wakifanya mazoezi
Shola Ameobi na Vincent Enyeama wakifanya mazoezi REUTERS/Edgard Garrido

Hii sio mara ya kwanza kwa Nigeria kugomea mazoezi kwa sababu ya marupurupu.

Timu nyingine ya Afrika ambayo ilijikuta katika hali hii ni pamoja Cameroon na Ghana ambao tayari wamebanduliwa nje ya michuano hii.

Ijumaa ni siku ya mapumziko na hii ndio ratiba ya michuano ya mwondoano kuanzia Jumamosi hii:
 

Jumamosi tarehe 28 Juni 2014

Brazil Vs Chile

Colombia Vs Uruguay

Jumapili tarehe 29 Juni 2014

Uholanzi Vs Mexico

Costa Rica Vs Ugiriki

Jumatatu tarehe 30 Juni 2014

Ufaransa Vs Nigeria

Ujerumani Vs Algeria

Jumanne tarehe 1 Julai 2014

Argentina Vs Uswizi

Ubelgiji Vs Marekani