BRAZIL 2014

Nigeria na Algeria kushuka dimbani kusaka ushindi muhimu

Nigeria inaingia uwanjani ikiwa na matumani ya kuwa timu ya nne kutoka barani Afrika kufika katika hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la dunia, baada ya Cameroon kufanya hivyo mwaka 1990, Senegal mwaka 2002 na Ghana mwaka 2010.

Matangazo ya kibiashara

Wachezaji wa Super Eagles wamekuwa wakikumbukwa na matatizo ya fedha na juma lililopita walisusia kufanya mazoezi kwa sababu hawakuwa wamelipwa na ilimlazimu rais Goodluck Jonathan kuwahakikishia kuwa watalipwa fedha zao zote.

Kocha Stephen Keshi atakuwa anamtegea mshambulizi Ahmed Musa ambaye alionesha kiwango cha juu katika mchezo dhidi ya Argentina juma lililopita.

Keshi pia anamtegemea kipa mwenye uzoefu mkubwa Vincent Enyeama, kuokoa mashambulizi kutoka kwa upande wa Ufaransa lakini huduma za Michael Babatunde zitakosekana kwa sabbau anauguza jeraha ila mshambulizi Victor Moses aliyekosa mechi iliyopita kwa sababu ya jeraha huenda akaanza leo.

Mshambulizi wa Nigeria  Peter Odemwingie.
Mshambulizi wa Nigeria Peter Odemwingie. REUTERS/Michael Dalder

Naye kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps anatarajiwa kumwanzisha kiungo wa kati Yohan Cabaye baada ya kumaliza adhabu ya kukosa mechi moja.

Beki Mathieu Valbuena naye anatarajiwa kuanza mchuano wa leo kuimarisha ngome ya le Blues na kuchukua nafasi ya Mamadou Sakho ambaye ana jeraha la paja.

Ufaransa inatafuta ubingwa wa mwaka huu baada ya kushinda taji hilo mwaka 1998 walipokuwa wenyeji.

Mshambulizi wa Ufaransa Karim Benzema akifanya mazoezi
Mshambulizi wa Ufaransa Karim Benzema akifanya mazoezi Reuters

Thathmini fupi
 

Ufaransa
Mara ya mwisho Nigeria kuifunga Ufaransa ilikuwa ni mwaka 2009 wakati wa mchuano wa Kimataifa wa kirafiki walipoifunga bao 1 kwa 0 katika mji wa St Ettinne.

Ufaransa, wamefungwa katika michuano miwili ya kombe la dunia na timu za Afrika mwaka 2002 walifungwa na Senegel na Afrika Kusini 2010.

Hata hivyo, Ufaransa imekuwa na rekodi nzuri katika michuano ya kombe la dunia mwaka 1958, 1982, 1986, 1998 walipokuwa mabingwa na 2006. Miaka hiyo yote walifika katika hatua ya nusu fainali.

Karim Benzema ni mchezaji wa kuangaliwa katika mchuano wa leo na amefunga mabao 9 katika michuano tisa aliyoicheza timu yake na tayari ameifungia Ufaransa mabao 3 katika michuano ya mwaka huu ya kombe la dunia.

Nigeria

Ikiwa Nigeria itafuzu katika hatua ya robo fainali, itakuwa mara ya kwanza kufanya hivyo katika historia yake ya michuano ya kombe la dunia.

Katika mechi 11 ya kombe la dunia walizocheza, wamefanikiwa kupata ushindi mmoja tu.

Beki Joseph Yobo ni wa kuangaliwa katika mchuano huu na ameweka historia kwa kuwa mchezaji aliyeichezea timu yake mara nyingi zaidi.

Yobo aliichezea nchi yake mchuano wake wa 100 juma lililopita na ikiwa atacheza leo basi atampita Jay Jay Okocha ambaye aliichezea timu yake mara tisa katika michuano ya kombe la dunia, huu utakuwa ni mchuano wake wa 10 katika michuano ya kombe la dunia.

Islam Slimani  mshambulizi wa Algeria akifunga bao dhidi ya Urusi
Islam Slimani mshambulizi wa Algeria akifunga bao dhidi ya Urusi Reuters

Algeria Vs Ujerumani.

Mchuano huu ni muhimu kwa Algeria ambao wanataka kuweka historia na wakati uo huo kulipiza kisasi dhidi ya Ujerumani kwa sababu miaka 32 iliyopita wakati wa michuano ya kombe la dunia mwaka 1982 katika hatua ya makundi, Algeria waliwafunga Ujerumani mabao 2 kwa 1 wakati huo wakifahamika kama West Germany matokeo ambayo yaliwashangaza wengi.

Algeria wangefuzu ikiwa Ujerumani wangefungwa na Austria au kuifunga Austria zaidi ya mabao 2 katika mechi ya mwisho lakini, Ujerumani waliwafunga Austria bao 1 kwa 0 na kuizuia Algeria kufika katika hatua ya 16 bora.

Wakati wa mechi hiyo, hakuna timu iliyokuwa inashambulia wala kutengeneza nafasi za kupata bao baada ya bao hilo kufungwa, na mwisho wa mechi hiyo, Ujerumani na Austria walifuzu katika hatua ya mwondoano kwa sababu walikuwa na mabao zaidi dhidi ya Algeria.

Kocha wa Algeria Vahid Halilhodzic anasema wachezaji wake wamekuwa wakilijadili suala hili na limeonekana kuwapa motisha kuelekea mchuano wa leo mshambulizi Islam Slimani anatarajiwa kuongoza mashambulizi.

Hii ndio mara ya kwanza kwa Algeria kufika katika hatua ya mwondoano.
Mara ya mwisho Algeria na Ujerumani kukutana ilikuwa ni mwaka 1982.

Algeria wameishinda Ujerumani mara mbili mwaka 1982 walipata ushindi wa mabao 2 kwa 1 katika michuano ya kombe la dunia na mwaka 1964 wakati wa mchuano wa kirafiki waliliishinda Ujerumani mabao 2 kwa 0.

Mario Götze  akifanya mashambulizi dhidi ya Ghana
Mario Götze akifanya mashambulizi dhidi ya Ghana REUTERS/Mike Blake

Naye Kocha wa Ujerumani Joachim  Low anatarajiwa kumpanga Mario Gotze baada ya mchezaji mwingine wa kutegemewa Lukas Podolski kupa ta jeraha wakati wa mchuano wa Ujerumani na Marekani juma lililopita.

Wachezaji wengine wa kutegemewa ni pamoja na mshambulizi Thomas Muller, Miroslav Klose na beki Jerome Boateng ambaye licha ya kuwa na jeraha la paja anatarajiwa kucheza leo hii.