SOKA

Afrika Mashariki na Kati yafanya vizuri katika michuano ya soka barani Afrika

Vlabu vinne vya soka kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati vimefanikiwa kufuzu katika mzunguko wa kwanza kuwania ubingwa wa klabu bingwa barani Afrika baada ya kupata ushindi mwishoni mwa juma lililopita katika viwanja mbalimbali barani Afrika.

Matangazo ya kibiashara

Timu hizo ni pamoja na Al Hilal ya Sudan, Al-Merrikh pia ya Sudan, Gor Mahia ya Kenya na APR ya Rwanda.

Mbali na michuano ya klabu bingwa barani Afrika mwishoni mwa juma lililopita, pia kulikuwa na michuano ya hatua ya awali ya kuwania taji la Shirikisho.

Al-Ahly Shendi ya Sudan, Rayon Sports ya Rwanda, URA ya Uganda na Yanga ya Tanzania pia zimefuzu katika mzunguko wa kwanza.

Katika michuano ya klabu bingwa, Al Hilal walifuzu baada ya kupata ushindi dhidi ya KMKM ya Zanzibar ya mabao 2 kwa 1 ugenini na nyumbani na watamenyana na Big Bullets ya Malawi.

Al-Merrikh waliwahakikishia mashabiki wao jijini Khartoum kuwa wanalenga kunyakua ubingwa wa mwaka huu baada ya kuwashinda Azam FC ya Tanzania bara kwa jumla ya mabao 5 kwa 0 na sasa watamenyana na Kabuscorp ya Angola.

Gor Mahia ya Kenya itamenyana na AC Leopards ya Congo Brazavile, baada ya kufuzu kutokana na bao la ugenini licha ya kufungwa na CNaPS Sport ya Madagascar kwa mabao 3 kwa 2, na ushindi wa bao 1 kwa 0 walililopia jiji Nairobi liliwasaidia kusonga mbele.

APR ya Rwanda wao watamenyana na mabingwa mara nane wa taji hili Al Ahly ya Misri baada ya kuwashinda Liga Desportiva de Maputo ya Msumbiji mabao 2 kwa 1.

Kaimu kocha wa APR Vincent Mashami amesema klabu yake inaweza kuwashinda mabingwa hao wa zamani wa Afrika na kueleza kuwa, Al Ahly sio klabu kutoka mbinguni.

Michuano hiyo itachezwa katikati ya mwezi huu na mwanzoni mwa mwezi ujao wa Aprili.

Katika michuano ya kuwania taji la Shirikisho, Al-Ahly Shendi ya Sudan itachuana na FC MK Etanchette ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rayon Sports ya Rwanda itapambana na Zamalek ya Misri, URA ya Uganda dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Yanga FC ya Tanzania bara itachuana na FC Platinum ya Zimbabwe nyumbani na ugenini.

Azam FC ya Tanzania bara na Sofapaka FC ya Kenya wawakilishi wengine wa Afrika Mashariki na Kati walibaduliwa nje ya michuano hii ya Shirikisho.