SOKA-UGANDA-MSUMBIJI

Milutin Sredojevic ajiuzulu

Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Uganda Mserbia Milutin Sredojevic amejiuzulu.
Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Uganda Mserbia Milutin Sredojevic amejiuzulu. FADEL SENNA / AFP

Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Uganda Mserbia Milutin Sredojevic amejiuzulu baada ya timu ya taifa yenye wachezaji wasiokuwa na zaidi ya umri wa miaka 23 kufungwa na Msumbiji mwishoni mwa juma lililopita.

Matangazo ya kibiashara

Uganda ilikuwa inatafuta tiketi ya kufuzu katika michuano ya Afrika itakayofanyika nchini Congo Brazaville mwezi Septemba mwaka huu, na katika mchuano wa mwisho mwa juma uliochezwa jijini Kampala, Msumbiji waliwashinda wenyeji mabao 4 kwa 1 kupitia mikwaju ya penalti baada ya timu hizo mbili kutoka sare ya kutofungana.

Baada ya mchuano huo, klabu ya Sudan ya Al-Hilal ilitangaza kumwajiri Sredojevic, mwenye umri wa miaka 45 ambaye ana historia ya kuzifunza timu mbalimbali barani Afrika.

Sredojevic anachukua nafasi ya Mbelgiji Patrick Aussems.

Mashabiki wa soka nchini Uganda walikuwa na hasira wakati wa upigaji wa mikwaju ya penalti, na kurusha chupa na mawe ndani ya uwanja wa Nakivubo katikati ya jiji la Kampala.

Mbali na vurugu zilizozuka uwanjani, wengine walitaka kujiuzulu kwa kocha “Micho” pamoja na rais wa Shirikisho la soka FUFA Moses Magogo.

Licha ya Uganda kubanduliwa nje ya michuano hiyo ya kufuzu, Nigeria, Misri, Burundi na Sudan zimefuzu katika hatua ya mwisho.

Mataifa manane pamoja na wenyeji Congo watashiriki katika michuano hii.