TANZANIA-ZIMBABWE-DRC-MSUMBIJI-CAF-SOKA

Yanga yaiburuza Platnum kwa mabao 5-1

Mashindano ya shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika.
Mashindano ya shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika. CAF

Katika mchuano wa mashindano ya shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika uliyochezwa Jumapili Machi 15 mjini Dar es Salaam, Tanzania, kati ya Yanga kutoka Tanzania na Platnum ya Zimbabwe, Yanga imeibuka mshindi.

Matangazo ya kibiashara

Yanga imeinyeshea Platnum kutoka Zimbabwe mvua ya magoli 5-1, mchezo ambao ulipigwa mjini Dar es Salaam.

Kipindi cha kwanza kilimalizika, Yanga ikiongoza kwa mabao 2-1. hata hivyo katika kipindi cha pili Yanga ilikuja juu na kuongeza mabao matatu.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Mrisho Ngasa (mabao mawili), Haruna Niyonzima (bao moja ), Salum Teleta (bao moja) na Amisi Tambwe (bao moja).

Platnum haikuweza kuliona lango la Yanga katika kipindi cha pili. Hadi kipenga cha mwisho timu hiyo ilijikuta ikiambulia bao moja tu ililofunga katika kipindi cha kwanza.

Yanga ambayo ni timu pekee iliyobakia kwenye mashindano ya shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika kutoka Tanzania, imeendelea kuweka matumaini ya kusonga mbele baada ya kuinyeshea mvua ya magoli Platnum ya Zimbabwe.

Katika michezo mingine ya mashindano hayo ya shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika, Vita Club kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iliifunga Ferrroviario Beira kutoka Msumbiji mabao 3-0, huku Orlando Pirates ya Afrika kusini ikiiadhibu URA ya Uganda kwa mabao 2-1.