KENYA

FIFA kuisaidia Kenya kutatua mzozo wa soka

Maofisa wa Shirikisho la soka duniani FIFA wapo jijini Nairobi nchini Kenya, kujaribu kutatua mvutano kati ya Shirikisho la soka nchini huo FKF na kampuni ya KPL kuhusu ni nani asimamie ligi kuu ya soka nchini humo msimu huu.

Matangazo ya kibiashara

Mvutano kati ya FKF na KPL ulianza mwishoni mwa mwaka jana baada ya FKF kupendekeza kuwa msimu wa mwaka 2015, uwe na vlabu 18 badala ya 16 kama ilivyozoeleka pendekezo ambalo lilikataliwa na KPL.

Uongozi wa KPL ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Jack Oguda, unasema ni vigumu kuwepo kwa vlabu 18 kwa sasa kwa sababu wamekwisha afikiana na wafadhili wa kituo Supersport kuwepo kwa timu 16 na mabadiliko yoyote yanaweza kusababisha mgogoro kati yao na wafadhili hao .

Ujumbe wa FIFA unaongozwa na rais wa Shirikisho la soka nchini Ghana, Kwesi Nyantakyi na Mkuu wa FIFA kuhusu maswala ya maendeleo eneo la Afrika Mashariki na Kusini Ashford Mamelodi.

Mwenyekiti wa FKF Sam Nyamweya amesema ana matumaini kuwa suluhu litapatikana kati yao na wasimamizi wa ligi ya KPL baada ya mazungumzo hayo na wawakilishi wa FIFA.

“Tuliifahamisha FIFA kuhusu mvutano huu unaoendelea, na nina imani kuwa suluhu litapatikana,”. alisema.

FKF inapendekeza kwa sasa kuwe na madaraja mawili ya ligi nchini Kenya, daraja la FKF na KPL lakini msimu ujao kuwe na ligi moja ili kumaliza mvutano huu, pendekezo ambalo litajadiliwa katika kikao hicho.

Majuma kadhaa yaliyopita, viongozi wa soka nchini Kenya walikwenda Mahakamani jijini Nairobi kutaka kusimamishwa kwa ligi ya KPL, lakini Mahakama ilitupilia mbali ombi hilo.

Nchini Kenya kwa sasa kuna ligi mbili zinazoendelea kwa wakati mmoja, ligi ya KPL na ile ya Shirikisho la soka FKF.

FKF juma lililopita walitia saini mkataba wa miaka mitatu na kituo cha Runinga cha Azam ili mechi zao zimeperushwe moja kwa moja kutoka viwanja mbalimbali nchini Kenya.