CAF

Nigeria mabingwa wa soka baina ya vijana chipukizi barani Afrika

Timu ya taifa ya soka ya Nigeria yenye wachezaji wasiozidi miaka 20 ndio mabingwa wa soka barani Afrika.

Timu ya taifa ya vijana chipukizi wa  Nigeria
Timu ya taifa ya vijana chipukizi wa Nigeria CAF
Matangazo ya kibiashara

Nigeria walinyakua ubingwa huo baada ya kuwafunga wenyeji Senegal bao 1 kwa 0 katika fainali ngumu iliyochezwa mwishoni mwa juma lililopita jijini Dakar.

Ushindi wa Nigeria katika Makala haya ya 20, unawafanya kuwa na mataji 7 tangu kuanza kwa michuano hii baina ya chipukizi barani Afrika.

Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Ghana iliyoifunga Mali bao 3 kwa 1.

Licha ya kushiriki katika michuano ya Afrika , mataifa hayo manne mabingwa Nigeria, Mali, Ghana na Senegal yamefuzu katika michuano ya kombe la dunia baina ya vijana yatakayofanyika mwezi wa Juni mwaka huu nchini New Zealand.

Mataifa manane yalishiriki katika michuano hiyo iliyoanza tarehe nane mwezi huu.
Mataifa hayo ni pamoja na mabingwa Nigeria, Senegal, Ivory Coast na Congo Brazavile ambao walikuwa katika kundi A.

Mali, Ghana, Afrika Kusini na Zambia walikuwa katika kundi la B, huku Afrika Kusini na Zambia wakirudi nyumbani baada ya kushindwa kufanya vizuri katika michuano hiyo.

Michuano hii imemalizika huku Musa Muhammed wa Nigeria akiwa mfungaji bora kwa kutikisa nyavu mara 4.

Mataifa 25 yatashiriki katika kombe la dunia na Ghana wamejumuishwa katika kundi la B, na Argentina Panama na Austria.

Mali nayo ipo katika kundi moja na Qatar, Colombia na Ureno, huku Senegal wakipangiwa katika kundi moja na Mexico, Uruguay na Serbia.

Mabingwa Nigeria wapo katika kundi moja na Brazil, Korea Kaszini na Hungary.