KENYA-MICHEZO-RIADHA

Isaiah Kiplagat awania Uwenyekiti wa IAAF

Rais wa Shirikisho la riadha nchini Kenya Isaiah Kiplagat amesema ataachia wadhifa huo kuanzia tarehe 1 mwezi ujao ili kutafuta uungwaji mkono wa kuchaguliwa kuwa Makamu wa rais wa Shirikisho la riadha duniani IAAF.

Raia watatu wa Kenya katika mashindano ya mabingwa wa Afrika wa Riadha mwaka 2010.
Raia watatu wa Kenya katika mashindano ya mabingwa wa Afrika wa Riadha mwaka 2010. Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kiplagat ambaye amekuwa Mwenyekiti wa Shirikisho hilo kwa miaka 22 sasa na pia mwanachama wa Kamati kuu ya IAAF, anawania wadhifa wa Umakamu wa urais wakati wa uchaguzi huo utakaofanyika mwezi Agosti jijini Beijing nchini China.

“ Nimefanya kazi katika Shirikisho hili kama Mwenyekiti kwa miaka mingi. Nafikiri kuwa huu ndio wakati wa mimi kuondoka na kumwachia mtu mwingine kuendelea”, Kiplagat amewaambia wanahabari jijini Nairobi.

“ Ntaachia uongozi kuanzia tarehe 1 mwezi Mei, na nimemteua Naibu wangu Jakcon Tuwei kuwa Mwenyekiti mpya na Paul Mutwii naibu wake”, ameongeza Kiplagat.

Kiplagat amesema kuwa ana matumaini ya kuchaguliwa katika wadhifa huo ambao ulikuwa unashikiliwa na Sebastian Coe ambaye anawania wadhifa wa Mwenyekiti wa IAAF kuchukua nafasi ya Lamine Diack raia wa Senegal ambaye anastaafu baada ya kuchaguliwa mwaka 1999.

Mgombea mwingine anayetafuta Urais wa IAAF ni Sergei Bubka kutoka Ukraine.