KENYA-SOKA-GOR MAHIA

Kujitolea na nidhamu vyaisaidia Gor Mahia

Mabingwa mara 14 wa ligi kuu ya soka nchini Kenya Gor Mahia wanaendelea kufanya vizuri katika ligi ya KPL tangu waliposhinda taji hili mara mbili mfululizo mwaka 2013 na 2014.

Nairobi,mji mkuu wa Kenya.
Nairobi,mji mkuu wa Kenya. AFP PHOTO / SIMON MAINA
Matangazo ya kibiashara

Ilikuwa ni safari ndefu toka mwaka 1995 hadi mwaka 2013 walipomaliza ukame wa ubingwa wa soka nchini Kenya.

Mwaka 2013 umekuwa mwamko mpya kwa Gor Mahia inayofahamika kwa jina maarufu Kogalo.

Wachezaji wamekuwa wakionesha ukakamavu na kucheza kwa kujitolea ili kulinda heshima yao na ya maelfu ya mashabiki wao.

Toka mwaka 2013 kujitolea na nidhamu vimewasaidia sana wachezaji kucheza vizuri na kwa moyo ili kurejesha historia nzuri ya klabu hii kama ilivyokuwa miaka ya 70 na 80 .

Wengi wanatamani kuiona ile Gor Mahia ya mwaka 1987 iliyoshinda taji la soka barani Afrika CAF walipoishinda Espérance Sportive de Tunis ya Tunisia katika mchuano wa fainali.

Kujitolea na nidhamu waliyonayo wachezaji wa Gor Mahia kumechangia pakubwa na mchezaji wa zamani na aliyekuwa kocha James Aggrey Siang'a  mwaka 2009 aliyekifumua kikosi hicho kwa kuwasajili wachezaji chipukizi.

Kuwasili kwa makocha wa kigeni kama  Zdravko Lugarusic, Bobby Williamson na sasa Frank Nuttall kumeisadia Gor Mahia kuinuka.

Nidhamu ya wachezaji wakiwa uwanjani imeimarika mno. Wanajitahidi sana kucheza kwa utulivu na kuonana na pasi zimekuwa za kuonana. Kasi ya mchezo pia imeongezeka na ni mara chache sana utawaona wachezaji wakilaumiana kama ilivyokuwa zamani.

Inasadikiwa kuwa kocha Nuttal amewaambia wachezaji kuwa siri ya mafanikio ni kushirikiana uwanjani, kutokuwa wachoyo na mpira na kucheza kwa moyo.

Msimu uliopita mwa 2014, Gor Mahia haikuwa na mfadhili lakini licha ya changamoto za kifedha zilizoikumba, ilinyakua ubingwa. Ilipoteza michuano minne tu, ikatoka sare mara 9 na kushinda michuano 17 kati ya mechi 30 walizohitajika kucheza.

Mfano wa kujitolea unaweza kuonekana kwa kipa Jeremy Onyango ambaye alipokuwa uwanjani alicheza kwa moyo, bila masihara na kuwahimiza wenzake kutumia ipasavyo nafasi wanazozipata mbele ya lango na kupata mabao.

Hili linaonekana pia msimu huu wa mwaka 2015, kati ya mechi saba walizocheza, Gor Mahia wameshinda mitano na kutoka sare miwili na hawajapoteza mchuano wowote.

Mashabiki wa Gor Mahia “The Green army” nao wamekuwa na wanaendelea kuwa na mchango mkubwa katika klabu hii kwa kufika uwanjani kwa maelfu na kuwashangilia wachezaji, hali ambayo imewapa motisha vijana hawa.

Ikiwa wachezaji wa Gor Mahia wataendelea kujitolea na kucheza kwa nidhamu kama ilivyo sasa, licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili mfano fedha, na kadhalika. Inaaminika kuwa Gor Mahia inatabiriwa kushinda tena ligi kuu ya KPL msimu huu.