FIFA-BLATTER-KUJIUZULU-SHERIA

Hatima ya CAF baada ya kujizulu kwa Sepp Blatter

Sepp Blatter wakati wa mkutano na vyombo vya habarikwenye makao makuu ya FIFA, Zurich,Mei 9 mwaka 2011.
Sepp Blatter wakati wa mkutano na vyombo vya habarikwenye makao makuu ya FIFA, Zurich,Mei 9 mwaka 2011. REUTERS/Arnd Wiegmann

Uamuzi wa Joseph Sepp Blatter kutangaza kujiuzulu kwenye fadhifa wa rais wa Shirikisho la soka duniani FIFA siku chache tu baada ya kuchaguliwa umeushangaza ulimwengu wa soka hasa bara la Afrika na Asia waliompigia kura kwa wingi.

Matangazo ya kibiashara

Hata kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa mwezi uliopita, viongozi wa Afrika walitangaza kwa kauli moja kuwa watampigia kura Blatter ili aendelee kuongoza soka duniani.

Amaju Pinnick rais wa Shirikisho la soka nchini Nigeria NFF alinukuliwa akisema kuwa Blatter ndiye mtu wa pekee ambaye amehakikisha kuwa Afrika inapata maendeleo ya soka.

“ Hatuwezi kuamini mtu ambaye anatuahidi kutufanyia kazi, tutamchagua Blatter kwa sababu tumeona yale aliyotufanyia”, Pinnick amesisitiza.

Rais wa Shirikisho la soka barani Afrika Issa Hayatou alionekana mwenye furaha kubwa baada ya Blatter kushinda na hata baada ya hotuba yake, viongozi wa soka barani Afrika na mataifa ya Caribbean walimzingira Blatter na kumpongeza kwa kupata ushindi.

Je, kujiuzulu kwa Blatter mwenye umri wa miaka 79 kunaashiria mabadiliko ya soka pia barani Afrika ? Je, wakati wa Hayatou ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka 1986 inafikia ukingoni ? Haya ni maswala yanayoendelea kuulizwa.

Kwanini Blatter ajizulu wakati huu ?

Shinikizo kutoka kwa maafisa wa Shirika la ujasusi la FBI kuwachunguza maafisa saba waliokamatwa kwa tuhma za ufisadi zimemkosesha usingizi.

Ripoti zinasema kuwa tayari FBI wameanza kumchunguza Blatter ikiwa anahusika kwa namna yoyote na tuhma hizo.

Blatter amesema hawezi kuendelea kuongoza FIFA kwa sababu haungwi mkono na kila mmoja. Ameahidi mabadiliko makubwa kabla ya kuondoka rasmi mwezi Desemba au kabla ya mwezi Machi mwaka ujao.

Nani anaweza kumrithi Blatter ?

Ni swali ambalo kila mmoja anajiuliza. Wachambuzi wa soka wanasema FIFA inamtafuta mtu ambaye ataweza kuliunganisha tena Shirikisho hilo baada ya kuonekana kugawanyika wakati wa uongozi wa Blatter.

Suala jingine kuu la kujiuliza, je wale waliompigia kura watafanya hivyo kwa yule atakayependelewa na Blatter ikiwa atafanya hivyo ?

Rais wa Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA Michel Plattini ni miongoni mwa watu wanaopewa kipau mble kuwania nafasi hii, lakini ikiwa atafanya hivyo itamlazimu atafute mbinu za kupata kura kutoka nje ya bara la Ulaya.

Mtu mwingine ni Mwanamfalme wa Jordan Hussein Bin Ali aliyepambana na Blatter katika uchaguzi uliopita na kushindwa.

Jeffrey Webb, ambaye pia alionekana kuwa katika nafasi nzuri ya kuwania wadhifa huo baada ya Blatter inavyoonekana hatafanya hivyo kwa sababu ni mmoja wa washukiwa wa ufisadi .

Ipi hali ya baadaye ya FIFA ?

Mkuu wa idara ya kuhakikisha kuwa kanuni za FIFA zinaheshimiwa Domenico Scala, amesema kwa sasa Shirikisho hilo linahitaji mabadliko makubwa.

Changamoto ni kwamba mabadiliko yoyote ni lazima yapigiwe kura na wajumbe wa Fifa kutoka kote duniani hali ambalo tumeshuhudia wakati mwingine yakipingwa.

Hata hivyo shinikizo hizi za ufisaidi kutoka kwa FBI na wafadhili mfano kampuni ya Cocacola huenda yakaleta mabadiliko.

Scala pia anasema mabadiliko muhimu ni kuwepo kwa mihula ya kuhudumu katika shirikisho hilo, kwa sasa hakuna muda maalum wa rais wa FIFA kumaliza muda wake.

Mfano Blatter amekuwa katika uongozi wa FIFA kwa miaka 17.

Pamoja na hayo, huenda pia ikiwa wajumbe watapitisha kwa mara ya kwanza, mshahara wa rais wa FIFA utawekwa wazi.

Hatima ya kombe la dunia nchini Urusi na Qatar.

Urusi itakuwa mwenyeji wa kombe la dunia mwaka 2018 huku Qatar ikiandaa michuano hiyo mwaka 2022.

FIFA chini ya uongozi wa Blatter imeendelea kupata lawama kuhusu namna nchi hizo zilivyopata nafasi hiyo huku kukiwepo ya madai kuwa kulikuwa na utoaji wa rushwa tuhma ambazo zimekanushwa na FIFA.

Marekani na Uingereza zimejitokeza waziwazi na kusema kutoridhishwa kwao na michuano hii kupelekwa nchini Urusi na Qatar.

Swali kubwa linalooulizwa je shinikizo kutoka mataifa hayo zimeweza kusababisha Qatar kupokonywa nafasi hiyo au hata Urusi ?

Rais wa Urusi Vladimir Putin tayari amedokeza wazi kuwa Marekani na Uingereza hazikufurahishwa na hatua ya kombe la dunia kuletwa nchini mwake.

Hata hivyo, wachambuzi wa soka wanaona kuwa huenda isiwe rahisi kuinyanganya Urusi michuano hiyo kwa sababu muda uliosalia ni mfupi sana kuanza maandalizi mengine ya kombe la dunia.

Afrika Kusini yakana kutoa rushwa

Serikali ya Afrika Kusini imejitokeza kupinga tuhma kuwa ilitoa rushwa ili kupewa nafasi ya kuandaa michuano ya kombe la dunia mwaka 2010.

Waziri wa Michezo Fikile Mbalula amesema Dola Milioni 10 zilizotolewa na Shirikisho la soka nchini humo ili kusaidia maendeleo ya soka katika nchi za Carrebian chini ya Shirikisho la soka la eneo hilo CONCACAF.

Viongozi wa Mashtaka nchini Marekani wanadai kuwa, Afrika Kusini ilitoa fedha hizo na kumpa Naibu rais wa FIFA Jack Warner ambaye wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa CONCACAF kuwahonga wajumbe ili waipigie kura Afrika Kusini.

Afrika Kusini inasema Marekani ishughulike na FIFA bali sio kuwahusisha katika suala ambalo halina ukweli.