ARSENAL-CHELSEA-LIGI KUU YA UINGEREZA

Mlinda mlango wa zamani wa Chelsea, Peter Cech asaini mkataba kuitumikia klabu ya Arsenal msimu ujao

Mlinda mlango mpya wa Arsenal, Peter Cech
Mlinda mlango mpya wa Arsenal, Peter Cech ArsenalFC Web

Aliyekuwa mlinda mlango wa klabu ya Chelsea ya nchini Uingereza, Peter Cech hatimaye ametia saini mkataba mpya wa kuitumikia klabu ya Arsenal katika msimu uhao wa ligi kuu ya Soka nchini Uingereza. 

Matangazo ya kibiashara

Tangazo la Cech kujiunga na klabu ya Arsenal lilichapishwa kwenye mtandao wa klabu hiyo, tangazo ambalo limesema kuwa Cech amesaini mkataba wa muda mrefu na klabu hiyo kwa dau ambao halikuwekwa wazi.

Cech raia wa Jamhuri ya Czech ameichezea Chelsea mechi zaid ya 400 katika kipindi cha miaka 11 aliyoitumikia klabu hiyo ya jiji la London, lakini hivi karibuni alijikuta akikaa benchi muda mrefu baada ya kocha wake kumtumia zaidi kinda, Thibaut Courtois.

Cech baada ya kusaini mkataba wake, amesema kuwa anafurahi kujiunga na klabu ya Arsenal na anasubiri sasa kujiunga na kambi ya timu hiyo kwaajili ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi.

Katika kipindi chake na klabu ya Chelsea, Peter Cech amepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kushinda mataji manne ya ligi kuu ya Uingereza, vikombe vinne vya kombe la FA na kombe la klabu bingwa Ulaya mwaka 2012.

Wakati tayari akiwa ameshatia saini kuitumikia Arsenal msimu ujao, kabla ya kuondoka aliyekuwa nahodha wake, John Terry alisema kuwa Cech ataenda kuimarika zaidi na klabu ya Arsenal ambao walimaliza kwenye nafasi ya tatu kwenye msimu wa ligi uliomalizika.