CHELSEA-ARSENAL-LEAGUE CUP

Chelsea na Arsenal zaaga Kombe la Ligi

Kocha wa Chelsea Jose Mourinho akimuelekeza Eden Hazard, nyota wa Chelsea aliyepoteza mkwaju wa penalti
Kocha wa Chelsea Jose Mourinho akimuelekeza Eden Hazard, nyota wa Chelsea aliyepoteza mkwaju wa penalti REUTERS

Nyota ya Mourinho imendelea kufifia msimu huu baada ya vijana wake kuondolewa katika michuano ya Kombe la Ligi (la League Cup) na Stoke City kupitia mikwaju ya penalti. Mechi hii ilichezwa Jumanne usiku Oktoba 27.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya Chelsea kudhibiti mpira katika kipindi cha kwanza ambacho hakikuzaa bao lolote, Stoke walitwaa uongozi kupitia Jon Walters dakika ya 52. Mechi hii ilipigwa katika uwanja wa Brittania.

Loic Remy aliwaokoa Chelsea, japo kwa muda alipofunga bao dakika ya 90, sekunde chache kabla ya mchezaji wa Stoke Phil Bardsley kufukuzwa uwanjani baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu.

Stoke walifunga mikwaju yao yote, lakini Eden Hazard akakosa mkwaju wake uliokuwa wa mwisho, ambao ulizimwa na kipa Jack Butland.

Mashabiki wa Stoke walifurahia sana ushindi wao na kusema kuwa Jose Mourinho ana mbwembwe zisiozaa chochote, wengine wakisema huenda akafutwa Jumatano asubuhi.

Chelsea walilazwa 2-1 na West Ham Jumamosi katika mechi ambayo Mourinho alifukuzwa eneo wanakokaa makocha baada yake kumtafuta na kumzungumzia refa Jon Moss wakati wa mapumziko.

Wakati huo huo Arsenal wamebanduliwa katika michuano hiyo baada ya kuburuzwa kwa mambao 3-0 na Sheffield Wednesday. Mashabiki wa Arsenal wamebaini kwamba klabu yao haikuwa na bahati katika mchuano huo.

Itafahamika kwamba Arsenal waliwakosa wachezaji wake wawili viungo, ikiwa ni pamoja na Theo Walcott na Alex Oxlade-Chamberlain baada ya kuumia katika dakika 20 ya kipindi cha kwanza. Arsenal ilipata makombora mawili pekee yaliyolenga goli.