VIWANJANI MWAKA 2016

Baadhi ya matukio makubwa yanayotazamiwa kufanyika mwaka 2016

Uwanja wa soka wa Amahoro jijini Kigali, moja ya viwanjwa kutakochezwa michuano ya CHAN 2016.
Uwanja wa soka wa Amahoro jijini Kigali, moja ya viwanjwa kutakochezwa michuano ya CHAN 2016. AFP

Makala ya nne ya mashindano ya kuwania ubingwa wa Afrika katika mchezo wa soka baina ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani CHAN, yataanza kutimua vumbi tarehe 16 mwezi huu wa Januari hadi mwezi Februari tarehe 7.

Matangazo ya kibiashara

Michuano hii itafanyika nchini Rwanda.

Mataifa 16 yatashiriki katika michuano hii ambayo hufanyika kila baada ya miaka miwili tangu mwaka 2009.

Michuano hiyo itachezwa katika viwanja vinne, uwanja wa Amahoro, jijini Kigali, ulio na uwezo wa kuwakaribisha mashabiki elfu 30.

Uwanja wa Nyamirambo ambao pia upo jijini Kigali, uwanja wa Butare na ule wa Gisenyi.

Mataifa yaliyofuzu ni pamoja na wenyeji Rwanda, Uganda, DRC, Ethiopia, Zambia, Zimbabwe, Angola, Gabon, Cameroon, Nigeria, Niger, Ivory Coast, Mali, Guinea, Tunisia na Morocco.

Mkutano mkuu wa FIFA kufanyika Februari 2016

Nembo ya Shirikisho la kimataifa la Soka (FIFA) mbele ya shirikisho hilo mjini Zuric Oktoba 8, 2015.
Nembo ya Shirikisho la kimataifa la Soka (FIFA) mbele ya shirikisho hilo mjini Zuric Oktoba 8, 2015. AFP/AFP/Archives

Mkutano Mkuu wa Shirikisho la soka duniani FIFA usiokuwa wa kawaida utafanyika tarehe 26 mwezi ujao wa Februari katika Makao makuu ya Shirikisho hilo jijini Zurich nchini Uswisi.

Ajenda kuu ya Mkutano huu itakuwa ni kumchagua rais mpya wa FIFA kuchukua nafasi ya Sepp Blatter ambaye amepigwa marufuku ya kushiriki katika maswala ya soka kwa muda wa miaka minane kutokana na ufisadi katika Shirikisho hilo.

Wagombea wanaowania nafasi hiyo ni pamoja na:

Mwanamfalme wa Jordan Ali bin Hussein, Makamu wa rais wa FIFA.
Salman Bin Ibhrahim Al-Khalifa, rais wa Shirikisho la soka barani Asia.
Jerome Champagne aliyekuwa Mwanakamati katika Shirikisho la soka duniani FIFA
Tokyo Sexwale mfanyibiashara kutoka Afrika Kusini.
Gianni Infantino Katibu mkuu wa Shirikisho la soka barani Ulaya.

Michezo ya Olimpiki

Fainali ya mashindano ya mbio za mita 200 katika Michezo ya Olimpiki ya 2008.
Fainali ya mashindano ya mbio za mita 200 katika Michezo ya Olimpiki ya 2008. Adam Pretty/Getty Images

Mwezi Agosti utakuwa ni mwaka wa michezo ya Olimpiki duniani.

Michezo hii itafanyika wakati wa kipindi cha joto jijini Rio de Janeiro nchini Brazil katiya tarehe 5 hadi 21 mwezi huo wa Agosti.

Wanamichezo zaidi ya elfu 10 kutoka mataifa 206 ambayo ni wanachama wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki watashiriki katika michezo mbalimbali wakati wa mashindano hayo.

Michezo 28 itachezwa katika mashindano hayo ikiwa ni pamoja na mchezo wa raga kwa wachezaji saba kila upande na mchezo wa Golf.

Michezo hii miwili ilijumuishwa katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2009.

Viwanja 33 vitatumiwa kuandaa mashindano hayo katika miji ya Barra, Copacabana, Deodoro na Maracana.

Makala ya 15 ya kuwania taji la UEFA 2016

Barani Ulaya, kati ya tarehe 10 mwezi Juni hadi Tarehe 10 mwezi Julai, Ufaransa itakuwa mwenyeji wa makala ya 15 kuwania taji la soka la bara la Ulaya UEFA mwaka huu wa 2016.

Kwa mara ya kwanza katika mashindano haya, mataifa 24 yatashiriki kutoka mataifa 16 ambayo yamekuwa yakipambana katika mashindano haya tangu mwaka 1996.

Kutakuwa na makundi sita na kila kundi litakuwa na timu nne.

Ufaransa mwenyeji wa makala ya 15 ya kuwania taji la soka la bara la Ulaya UEFA mwaka  2016.
Ufaransa mwenyeji wa makala ya 15 ya kuwania taji la soka la bara la Ulaya UEFA mwaka 2016. REUTERS/Michaela Rehle

Itakuwa ni mara ya tatu kwa Ufaransa kuandaa mashindano haya baada ya kufanya hivyo mwaka 1960 na 1984.

Michuano hii itachezwa katika miji 10 na miongoni mwa miji hiyo ni pamoja na Paris, Nice, Saint-Denis, Saint-Étienne,  Toulouse.

Wenyeji wa mashindano haya Ufaransa wameshinda mara mbili: mwaka 1984 na 2000.

Mabingwa watetezi ni Uhispania ambao wameshinda mara mbili mfululizo taji hili: mwaka 2008 na 2014.