CHAN 2016-MAKUNDI

CHAN 2016: uchambuzi wa hatua ya makundi

Pembezoni mwa uwanja wa mpira wa Amahoro mjini Kigali, kabla ya mchuano kati ya Rwanda na Côte d'Ivoire kwa michuano ya CHAN 2016.
Pembezoni mwa uwanja wa mpira wa Amahoro mjini Kigali, kabla ya mchuano kati ya Rwanda na Côte d'Ivoire kwa michuano ya CHAN 2016. David Kalfa / RFI

Michuano ya soka kuwania ubingwa wa bara la Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani CHAN, inaendelea kupamba moto katika viwanja mbalimbali nchini Rwanda.

Matangazo ya kibiashara

Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tayari zimefuzu katika hatua ya robo fainali baada ya kuandikisha ushindi katika michuano yao miwili katika kundi A na B.

Kundi A

Wenyeji Rwanda, wamejumuishwa katika kundi moja na Ivory Coast, Morroco na Gabon.

Amavubi Stars wanaongoza kwa alama sita baada ya kushinda mchuano wao dhidi ya Côte d’Ivoire bao 1 kwa 0 na baadaye Gabon mabao 2 kwa 1.

Mchuano unaosalia kutamatisha kundi hili ni dhidi ya Morocco siku ya Jumapili.

Côte d’Ivoire ambayo ni ya pili katika kundi hili kwa alama tatu, iko katika nafasi nzuri ya kufuzu ikiwa itaishinda Gabon siku ya Jumapili.

Gabon pia ina nafasi nzuri ikiwa itashinda mchuano huo na kuomba kuwa Rwanda inaifunga Morroco au inatoka sare kwa sababu, Morroco nayo ina alama moja.

Kundi B

Mabingwa wa mwaka 2009, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaongoza kundi hili kwa alama sita baada ya kushinda michuano yake miwili dhidi ya Ethiopia kwa kuwafunga mabao 3 kwa 0 na kuifunga Angola mabao 4 kwa 2.

Mchuano wake wa mwisho kutamatisha kundi hili ni siku ya Jumatatu dhidi ya Cameroon katika uwanja wa Huye mjini Butare.

Cameroon ni wa pili katika kundi hili kwa alama 4 na mchuano wake na DRC ni muhimu kwa sababu inahitaji ushindi.

Ethiopia ambayo ina alama moja pia bado ina nafasi ya kusonga mbele ikiwa itaishinda Angola pia siku ya Jumatatu, ambayo tayari imeondolewa baada ya kufungwa mechi zake mbili .

Walia Ibex pia inaomba kuwa DRC inaishinda Cameroon.

Kundi C

Hadi sasa kundi hili linaongozwa na Nigeria ambayo ina alama 4.

Super Eagles iliishinda Niger mabao 4 kwa 1 katika mchuano wake wa kwanza lakini ikatoka sare ya bao 1 kwa 1 na Tunisia siku ya Ijumaa.

Mchuano wa mwisho wa Nigeria katika kundi hili utakuwa dhidi ya Guinea siku ya Jumanne juma lijalo katika uwanja wa Umuganda mjini Gisenyi.

Tunisia ambayo ni ya pili kwa alama 2 bado ina nafasi ya kufuzu ikiwa itaishinda Niger juma lijalo.

Niger na Guinea pia wana alama nafasi ya kufuzu.Guinea ina alama mbili huku Niger ikiwa na alama moja.

Siku ya Ijumaa, Guinea na Nigeria zilitoka sare ya mabao 2 kwa 2.

Kundi hili ni gumu kwa sababu hakuna aliye na uhakika wa kufuzu moja kwa moja.

Mshambuliaji wa Nigeria Chisom Chikatara anaongoza katika safu ya ufungaji wa mabao na hadi sasa ameifungia nchi yake mabao 3.

Kundi D

Michuano ya pili ya kundi hili inapigwa siku ya Jumamosi jioni katika uwanja wa Umuganda mjini Gisenyi.

Hadi sasa kundi hili linaoongozwa na Zambia kwa alama 3 ambayo iliishinda Zimbabwe kwa bao 1 kwa 0 mapema juma hili.

Mali na Uganda zina alama 1 baada ya kutoka sare ya mabao 2 kwa 2.

Jumamosi jioni, Zimbabwe wanamenyana na Mali na baadaye Uganda na Zambia.

Michuano ya kundi hili itachezwa siku ya Jumatano, Uganda itamenyana na Zimbabwe na Zambia itamaliza kazi na Mali.