CHAN 2016: ROBO FAINALI

CHAN 2016: timu 8 katika hatua ya robo fainali zafahamika

Timu ya taifa ya Rwanda, Novemba 2015.
Timu ya taifa ya Rwanda, Novemba 2015. AFP PHOTO / SALAH LAHBIBI

Mataifa manane yatakoyoshiriki katika hatua ya robo fainali ya michuano ya soka kuwania ubingwa wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani CHAN, yamefahamika.

Matangazo ya kibiashara

Michuano ya robo fainali itaanza kupigwa kuanzia mwishoni mwa juma hili na wenyeji Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinawakilisha ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mbali na Rwanda na DRC, mataifa mengine yaliyofuzu ni pamoja na Cameroon, Ivory Coast, Tunisia, Mali, Zambia na Guinea.

Mechi ya kwanza ya robo fainali itapigwa siku ya Jumamosi na mchuano wa kwanza utakuwa ni kati ya wenyeji Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika uwanja wa Amahoro jijini Kigali, kuanzia saa tisa mchana saa za Afrika ya Kati.

Mchuano huu unatarajiwa kuwavutia mashabiki wengi kutoka mataifa yote mawili ambao wote wanasema timu zao zitapata ushindi katika mchuano huo muhimu.

Mara ya mwisho kwa timu hizi kukutana, ilikuwa ni wakati wa mchuano wa kirafiki kabla ya kuanza kwa michuano hii ya CHAN , na Rwanda ilipata ushindi wa bao 1-0.

Cameroon na Ivory Coast nao watamenyana katika mchuano wa pili wa robo fainali kunzia saa 12 jioni saa za Afrika ya Kati, katika uwanja wa Huye mjini Butare.

Timu zote mbili zimekuwa zikitoana kijasho katika michuano mbalimbali na mara mwisho kukutana ilikuwa ni michuano ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka jana, ambako Cameroon waliifungwa na Ivory Coast bao 1 kwa 0.

Siku ya Jumapili, Tunisia itapambana na Mali na Zambia itachuana na Guinea ambayo inashiriki katika mashindano haya kwa mara ya kwanza.

Mechi za nusu fainali zitachezwa tarehe 3 na 4 mwezi ujao huku fainali ikichezwa tarehe 7 katika uwanja wa Amahoro jijini Kigali.

Hadi sasa Ahmed Akaichi kutoka Tunisia anaongoza katika safu ya ufungaji mabao kwa kutikisa nyavu mara 4, sawa na Chisom Chikatara kutoka Nigeria ambayo imendolewa katika michuano hii.