NEYMAR-BRAZIL-BARCELONA

Neymar kufunguliwa mashtaka mengine ya ukwepaji kodi nchini mwake, ni tofauti na yale anayokabiliwa nayo nchini Uhispania

Mshambuliaji wa FC Barcelona, Neymar da Silva Santos Júnior, anayekabiliwa na mashtaka ya ukwepaji kodi nchini Brazil na Uhispania
Mshambuliaji wa FC Barcelona, Neymar da Silva Santos Júnior, anayekabiliwa na mashtaka ya ukwepaji kodi nchini Brazil na Uhispania REUTERS/Sergio Perez

Waendesha mashtaka nchini Brazil, wamependekeza mshambuliaji wa kibrazil, Neymar afunguliwe mashtaka manne ya udanganyifu yanayohusiana na ukwepaji kodi wakati alipofanya uhamisho kujiunga na klabu yake ya sasa FC Barcelona, 2013.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye taarifa yao, waendesha mashtaka wa Brazil wanadai kuwa mchezaji huyo kwa kushirikiana na makampuni kadhaa, waliunda makampuni feki kwa lengo la kumfanya mshambuliaji huyo alipe kiasi kidogo cha kodi.

Waendesha mashtaka hao wanadai kuwa mashataka atakayofunguliwa mshambuliaji huyo ni ya muda wa miaka saba kuanzia mwaka 2006, ambapo mashtaka haya ni tofauti kabisa na yale anayokabiliana nayo mjini Spain, Uhispania.

Haya yanajiri ambapo Jumanne ya wiki hii mshambuliaji huyo alipandishwa kwenye mahakama ya mjini Madrid kujibu mashtaka yanayohusiana na udanganyifu anaozunguka mazingira ya usajili wake, huku yeye mwenyewe akikana kufanya kitu chochote kinyume cha sheria.

Waendesha mashtaka wa Brazil wanasema kuwa kesi inayomkabili Neymar ni wakatyi alipokuwa nchini humo na mapato ambayo aliyapata wakati akilipwa na vyanzo mbalimbali nchini humo.

Serikali inasema kuwa mashtaka hayo manne ya udanganyifu, yanahusu madai kuwa alifungua kampuni feki na kwamba hela alizokuwa akizipata wakati huo zilipaswa kutozwa kodi na kwamba kwakuwa alitumia makampuni alilenga kukwepa kodi binafsi ambayo ni tofauti na kama ukilipiwa na makampuni.

Hivi karibuni pia mshambuliaji mwenzake wa Argentina Lionel Messi naye alipandishwa kizimbani kujibu mashtaka ya ukwepaji kodi yanayomkabili yeye pamoja na baba yake.