SERIA A

Klabu ya Lazio yapigwa faini, mashabiki wake waonywa kuhusu kutoa ishara za kibaguzi

Beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly ambaye alioneshwa ishara za kibaguzi kwenye mechi yao ya Jumatano dhidi ya Napoli
Beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly ambaye alioneshwa ishara za kibaguzi kwenye mechi yao ya Jumatano dhidi ya Napoli Reuters

Klabu ya Lazio ya nchini Italia imetakiwa kulipa faini ya euro elfu 50 baada ya mechi yao dhidi ya Napoli Jumatano ya wiki hii kusimama kwa muda kutokana na mashabiki wake kuonesha ishara za kibaguzi.

Matangazo ya kibiashara

Lazio pia imetakiwa kufunga majukwa yake ya maeneo matatu ya uwanja wake wa nyumbani wa The Stadio Olimpico katika mechi zake mbili za nyumbani za seria A zinazokuja.

Mechi kati ya Lazio na Napoli ililazimika kusimamishwa kwa muda wa dakika tatu kipindi cha pili baada ya baadhi ya mashabiki wa Lazio kutoa maneno ya kibaguzi dhidi ya mlinzi wa Napoli, Kolidou Koulibaly.

Kwenye mchezo huo, vinara wa ligi ya Seria A, klabu ya Napoli ilifanikiwa kuchomoza na ushindi mwembamba wa bao 1-0, na kuendelea kuwafanya wakite mizizi katika usukuni wa msimamo wa ligi hiyo.

Koulibaly, beki wa kati raia wa Senegal, alimpongeza mwamuzi wa mchezo huo, Massimiliano Irrati kwa kusimamisha mchezo.

Mara baada ya mchezo huo, kocha mkuu wa Lazio, Stefano Pioli, alisema kama ingekuwa yeye asingesimamisha mchezo kwakuwa matamshi yalikuwa yakitolewa na mashabiki wachache ambao haamini kama walikuwa wabaguzi, na kuongeza kuwa timu yake ina wachezaji wa kiafirika na walikuwa hawazomewi.

Klabu ya Lazio mara kadhaa imekuwa ikipewa adhabu kutokana na mashabiki wake kukithiri kwa kutoa matamshi na kuonesha ishara za kibaguzi dhidi ya wachezaji wenye asili ya kiafrika.

February 10, 2015 mashabiki wa Lazio walionesha ishara za kibaguzi dhidi ya wachezaji wa Genoa na kufanya mechi hiyo kufutwa kabisa.