AFCON 2017-CHAD-TANZANIA-SOKA

AFCON 2017: Chad yajiondoa katika kinyang'anyiro

Mchezaji wa Misri Mohamed El Neny akiwafunga Chad bao la kwanza.
Mchezaji wa Misri Mohamed El Neny akiwafunga Chad bao la kwanza. REUTERS/Amr Abdallah Dalsh

Timu ya taifa ya Chad imechukua uamuzi wa kujiondoa katika kinyang'anyiro cha kufuzu kwa fainali ya mataifa ya Afrika inayotarajiwa kupigwa mwakani nchini Gabon.

Matangazo ya kibiashara

Shirikisho la soka la Chad limechukua uamuzi huo baada ya kukosekana kwa fedha ambazo zingelihudumia timu hiyo Chad katika michuano hiyo inayoendelea kupingwa katika viwanja mbalimbali.

Chad ingelicheza na Tanzania katika michuano ya kufuzu kwa fainali ya mataifa ya Afrika mwaka 2017 nchini Gabon inayoendelea hivi sasa.

Shirikisho la Soka la Chad limetuma barua kwa shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), ambapo mwenyekiti wa shirikisho la soka la Chad Moctar Mahamoud, amesema wanakabiliwa na ukosefu wa fedha za kufadhili safari ya kwenda Dar Salaam kwa mechi ya marudiano dhidi ya Taifa Stars Jumatatu hii, Machi 28, 2016.

Kufuatia uamuzi huo wa Chad, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limefuta matokeo ya mechi zote dhidi ya Chad, na hivyo kuitia mashakani timu ya taifa ya Tanzania.

Wakati huo huo CAF imewapiga marufuku Chad kutoka kwenye mashindano ya mwaka wa 2019 pamoja na kuitoza faini ya dola za Kimarekani 20,000.

Itakumbukwa kwamba katika kundi linaloundwa na Chad, Misri, Nigeria na Tanzania, timu ya taifa ya Chad imekua ikichukua nafasi ya mwisho katika kundi hili. Kwa sasa Tanzania inasalia na alama moja tu, huku timu ya taifa ya Misri ikiongoza kwa alama 4 na iwapo Nigeria watawashinda Misri Jumanne, Machi 29 watachukua nafasi ya kwanza.

Mpaka sasa Taifa Stars ya Tanzania wako mashakani, kulingana na sheria za shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambazo zinasema kuwa endapo kundi litakuwa na timu 3 basi timu inayoongoza pekee ndiyo inayosonga mbele.

Hayo yakijiri katika mechi zilizopigwa Jumapili hii katika muendelezo wa michuano ya kufuzu kwa fainali ya mataifa ya Afrika inayotarajiwa kupigwa mwakani nchini Gabon, Congo na Zambia wametoka sare ya kufungana 1-1, huku Benin wakiwafunga Sudan Kusini mabao 4-1.