AFCON 2017-MOROCCO-SOKA

Morocco yafuzu michuano ya AFCON 2017

CAF

Morocco imekuwa nchi ya kwanza kufuzu katika michuano ya soka ya Mataifa bingwa barani Afrika AFCON, itakayofanyika mwaka ujao nchini Gabon.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo ilikuja baada kuifunga Cape Verde mabao 2 kwa 0 katika mchuano muhimu uliopigwa Jumanne usiku mjini Marrakech.

Mshambuliaji wa Morocco Youssef El Arabi aliifungia timu yake mabao yote katika kipindi cha kwanza cha mchuano huo.

Vijana wa kocha Herve Renard raia wa Ufaransa ambaye aliwahi kuisaidia Cote d'Ivoire na Zambia kunyakua taji la AFCON, wanaongoza kundi lao la F kwa alama 12 baada ya kushinda mechi 4 walizocheza hadi kufikia sasa.

Misri na Senegal nazo zinakaribia kufuzu baada ya kushinda mechi zao muhimu.

Bao pekee la Ramadan Sobhy lilisaidia Misri kuwa na mguu mmoja nchini Gabon baada ya kuilaza Nigeria mjini Alexandria katika mchuano wa kundi G.

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Nigeria hawana uwezekano wa kufuzu kwa sababu kundi lao limesalia na timu tatu pamoja na Tanzania baada ya Chad kujiondoa.

Misri ambayo imeshinda taji la Afrika mara saba, ina alama 7 na inahitaji tu alama 1 kujihakikishia nafasi ya kucheza fainali hizo za mwaka 2017.

Matokeo ya kundi K, Senegal nayo ilijiweka katika nafasi nzuri baada ya kuifunga Niger mabao 2 kwa 1 yaliyofungwa na Moussa Konate na Papa Souare.

Senegal sasa inaongoza kundi la K kwa alama 12 mbele ya Burundi ambayo ina alama 6 baada ya kupata ushindi wa mabao 3 kwa 1 dhidi ya Namibia ugenini.

Uganda Cranes ikicheza nyumbani katika uwanja wa Naambole jijini Kampala, ilitoka sare ya kutofungana na kuacha kila mmoja na alama 7 katika kundi D.

Leopard ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nayo iliweka hai matumaini yake ya kufuzu baada ya kuifunga Angola mabao 2 kwa 0 ugenini.

Rwanda nayo iliishinda Mauritius mabao 5 kwa 0 huku Burundi ikiilemea Namibia mabao 3 kwa 1 jijini Windhoek.