BRAZIL-OLIMPIKI

Brazil: Mwenge wa Olimpiki wajiandaa kuwasili Brasilia

Mjii mkuu wa Brazilia unajiandaa kuupokea mwenge wa Michezo ya Olimpiki.
Mjii mkuu wa Brazilia unajiandaa kuupokea mwenge wa Michezo ya Olimpiki. AFP

Mwenge wa Olimpiki unatazamiwa kuwasili Jumanne hii katika mji mkuu wa Brazil, Brazilia. Mwenge huu unatazamiwa kuzunguka nchi nzima ya Brazil hadi wakati wa ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki mwezi Agosti. Hili ni tendo la kihistoria katika mji mkuu ambalo linaweza kuwa la mwisho kwa Dilma Rousseff kama rais wa Brazil.

Matangazo ya kibiashara

Kwa kipindi cha miezi mitatu,mwenge huu maarufu utasafirishwa kwa kutapitia katika njia za kimila za watu asilia wa Brazil, katika meli au mtumbwi, kwa farasi, kwa helikopta au kubebwa na mmoja kati ya waandamanaji 12,000 wanaoshiriki safari hiyo hiyo, hadi kuwasili kwake mnamo Agosti 5 katika uwanja wa Maracana mjini Rio, na kufungua Michezo ya Olimpiki ya kwanza katika ardhi ya nchi ya kusini mwa Marekani.

Mwenge huu uliyowashwa mwezi Aprili katika eneo la kale la Ugiriki la Olympie, utakabidhiwa Rais Rousseff katika makao makuu ya Ikulu, ambapo alikabidhiwa madaraka mwaka 2011 baada ya uchaguzi wake wa kwanza.

Rousseff huenda akaondoka kwenye wadhifa huo mwanzoni mwa juma lijalo iwapo Baraza la Seneti litapiga kura kwa idadi ndogo inayohitajika ya Maseneta kwa kufungua kesi yake kwa "uhalifu wa madaraka" katika utaratibu wa kumtimua mamlakani uliyoanzishwa dhidi yake.

Kama Maseneta watapiga kura hiyo, kuna uwezekano, kwa mujibu vyombo vya habari vya Brazil, kuwa Dilma Rousseff atatengwa kwa muda wa siku 180, na atakua akipokea tu nusu ya mshahara wake. Hata hivyo ataendelea kuishi katika makazi ya rais.

Itafahamika kwamba heluthi mbili ya kura za Maseneta inahitajika kwa kuweza kumuondoa mamlakani.