KENYA-FKF-SOKA

FKF yaanzisha utaratibu mpya kwa wachezaji

Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars.
Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars. youtube

Shirikisho la soka nchini Kenya (FKF), limetangaza rasmi kuanza kusimamia usajili wa wachezaji wote watakaocheza katika ligi zote nchini humo na wale watakaokuwa wanakwenda kucheza soka nje ya nchi.

Matangazo ya kibiashara

FKF inasema imeamua kuchukua jukumu hilo ili kusimamia kikamilifu kanuni za Shirikisho la soka duniani FIFA, na itaanza kutekelezwa kuanzia tarehe 2 mwezi Juni mwaka huu wakati wa usajili wa dirisha ndogo.

Kanuni ya FIFA, inasema kuwa Shirikisho la soka katika nchi husika itasimamia usajili wa wachezaji watakaocheza soka nchini humo lakini pia kufuatilia maendeleo yao.

FKF inasema mabadiliko haya yatasaidia usawa na urahihishaji wa usajili wa wachezaji hao.

Hata hivyo, uongozi wa soka nchini humo unasema usajili ambao ulifanywa na kampuni inayosimamia ligi KPL, utaendelea kutambuliwa na FKF.

Pamoja na hilo, wadau wote wanaoandaa michuano mbalimbali ya soka wametakiwa kulifahamisha Shirikisho la soka FKF.