Kenya yasubiri uamuzi wa IAAF na IOC
Imechapishwa:
Kenya inasubiri uamuzi wa Shirikisho la riadha duniani IAAF na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki IOC, kuhusu ushiriki wake katika mashindano ya Olimpiki mwezi Agosti mwaka huu nchini Brazil.
Hatua hii inakuja baada ya Shirika la Kimataifa linalopambana na matumizi ya dawa kuongeza nguvu mwilini kwa wachezaji (WADA), kuamua kwa kauli moja kuwa Kenya imeonyesha nia ya kutoshirikiana nalo katika vita hivi.
Ni habari ambayo imepokelwa kwa mshangao mkubwa na wakenya hasa wanariadha ambao tayari wameanza maandalizi ya kwenda kushiriki katika mashindano ya Olimpiki.
Uamuzi wa WADA umezua mjadala zaidi baada ya rais Uhuru Kenyatta wiki mbili zilizopita, kusaini sheria mpya iliyopitishwa na bunge kupambana na tatizo hilo.
Rais wa IAAF amenukuliwa akisema hatakuwa na lingine bali kuifungia Kenya kutoshiriki katika mashindano ya Kimataifa ikiwa itabainika kuwa haishirikiani na WADA.
Tangu mwaka 2012, wanariadha 40 wamepatikana na kosa la kutumia dawa zilizopigw amarufuku na WADA na 18 wamefungiwa kushiriki katika mashindano ya kimataifa na taifa ya riadha.