CAF-SOKA-AFRIKA

Mechi zapigwa katika viwanja mbalimbali

Michuano ya marudiano hatua ya mwondoano katika mchezo wa soka kuwania ubingwa wa taji la Shirikisho inachezwa leo na kesho katika mataifa mbalimbali barani Afrika.

TP Mazembe wakati wa michuano ya Kombe la Dunia la klabu 2015.
TP Mazembe wakati wa michuano ya Kombe la Dunia la klabu 2015. KAZUHIRO NOGI / AFP
Matangazo ya kibiashara

Mabingwa wa mwaka uliopita wa klabu bingwa barani Afrika TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, inamenyana na Stade Gabesien ya Tunisia.

Mazembe inayofuzwa na Mfaransa Hubert Velud, inakwenda katika mchuano huu ikiwa na ushindi wa bao 1 kwa 0 waliopata katika mchezo wa nyumbani mapema mwezi huu.

Mashabiki wa TP Mazembe wana imani kuwa klabu yao itawafuta machozi kwa kupata ushindi leo na kufuzu katika hatua ya makundi na kufika hadi fainali kunyakua ubingwa wa taji la Shirikisho baada ya kuondolewa katika michuano ya klabu bingwa.

Klabu hii yenye makao yake mjini Lubumbashi inajivunia wachezaji kutoka nchi mbalimbali kutoka barani Afrika kama Ghana, Côte d’Ivoire, Mali, Tanzania na Zambia. Mechi hii itapigwa kuanzia saa kumi na nusu jioni saa za Afrika Mashariki.

Mchuano mwingine unaochezwa leo ni kati ya Mo Bejaia ya Algeria mabyo itakuwa ugenini kumenyana na Esperance de Tunis ya Tunisia.

Mchuano wa kwanza, timu zote mbili zilitoka sare ya kutofungana. Mchuano huu utachezwa kuanzia saa mbili na nusu usiku saa za Afrika Mashariki.

Ratiba ya kesho na matokeo ya mzunguko wa kwanza:-

  • Stade Malien (Mali) vs FUS Rabat (Morroco) 0-0
  • Etoile du Sahel (Tunisia) vs CF Mounana (Gabon) 2-0
  • Al-Ahli Tripoli (Libya) vs Misr Lel Makkasa (Misri) 0-0
  • Al-Merrikh (Sudan) vs Kawkab Marrakech( Morroco) 1-0
  • Young Africans (Tanzania) vs Sagrada Esperanca (Angola) 2-0
  • Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) vs Medeama (Ghana) 3-1

Timu nane zitafuzu katika hatua ya makundi.