TFF-TANZNIA-SOKA

TFF kutoandaa michuano ya CECAFA

Shirikisho la soka nchini Tanzania linasema halitakuwa katika nafasi ya kuandaa michuano ya mwaka huu ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati CECAFA.

Mashabiki wa Taifa Stars wakati ilipokua ikifuana na Cote d'Ivoire  June 16 mwaka 2013.
Mashabiki wa Taifa Stars wakati ilipokua ikifuana na Cote d'Ivoire June 16 mwaka 2013. YouTube
Matangazo ya kibiashara

TFF ilikuwa imeahidi kuchukua nafasi ya Zanzibar iliyopewa jukumu hilo lakini ikajiondoa kwa ukosefu wa fedha.

Rais wa TFF Jamal Malinzi kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema, nchi yake haitaweza kuwa mwenyeji wa michuano hiyo kwa sababu ya msongamano wa mechi za Kimataifa jijini Dar es salaam baada ya Yanga FC kufuzu kucheza hatua ya makundi kuwania taji la Shirikisho.

“Shirikisho la soka nchini Tanzania, halitaandaa michuano ya klabu bingwa ya CECAFA mwaka 2016, kwa sababu ya msongamano wa ratiba ya kimataifa,” amesema Malinzi.

Michuano hii inafadhiliwa na rais wa Rwanda Paul Kagame, amekuwa akifadhili michuano hii tangu mwaka 2002, imepangwa kufanyika kuanzia katikati ya mwezi wa Julai hadi mwanzoni mwa mwezi wa Agosti.

Mwaka 2015 michuano hii inayofahamika kwa jina maarufu la Kagame Cup ilifanyika nchini Tanzania na wenyeji Azam FC wakayakua ubingwa kwa kuwashinda Gor Mahia ya Kenya mabao 2 kwa 0 katika fainali.

Tanzania imeandaa michuano hii mara tatu kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, hii ikitokana na idadi kubwa ya mashabiki wengi kujitokeza uwanjani.

Mara ya mwisho Kenya kuandaa michuano hii ilikuwa ni mwaka 2001, wakati huo vlabu vyote vya Kenya vilifika fainali, Tusker FC na Oserian Fastac na baada ya mikwaju ya penalti, Tusker wakanyakua taji hilo.