MESSI-HISPANIA

Messi apandishwa kizimbani mjini Barcelona, kujibu tuhuma za ukwepaji kodi

Lionel Messi, mchezaji wa FC Barcelona na timu ya taifa ya Argentina
Lionel Messi, mchezaji wa FC Barcelona na timu ya taifa ya Argentina Reuters/Miguel Vidal

Mshambuliaji wa kimataifa wa FC Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi, hii leo amepandishwa kizimbani kwenye mahakama moja mjini Barcelona kujibu mashtaka ya ukwepaji kodi yanayomkabili nchini Uhispania. 

Matangazo ya kibiashara

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 hivi sasa, aliwasili mahakamani hapo akiwa amevalia suti nyeusi, ambapo alishangiliwa na wakati fulani kuzomewa na watu waliofika mahakani kusikiliza kesi yake.

Lionel Messi ambaye alifika mahakamani hapo akiwa ameambatana na baba yake, Jorge Horacio Messi, wanatuhumiwa kwa kutumia mtandao wa makampuni kadhaa ya Belize na Uruguay kukwepa kulipa kodi inayifikia kiasi cha dola za Marekani milioni 4.6, fedha alizozipata kupitia uuzaji wa haki miliki ya picha yake kuanzia mwaka 2007 hadi 2009.

Mamia ya waandishi wa habari na wapiga picha walifurika mahakamani huku wakimzonga mchezaji huyo na baba yake wakati wakiingia mahakamani hapo wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Messi, mshindi mara tano wa tuzo ya mchezaji bora wa dunia "Ballon d'Or", alijikuta akizomewa na baadhi ya mashabiki waliomuita mwizi, huku baadhi ya waliongea na vyombo vya habari wamependekeza achukuliwe hatua kutokana na kukwepa kulipa kodi.

Awali maofisa wa mamlaka ya mapato nchini Ufaransa walipanda kizimbani na kuhojiwa na waendesha mashtaka kwenye kesi hiyo hata kabla ya Messi mwenyewe kuwasili. Kesi hii inatarajiwa kutamatika Ijumaa ya wiki hii.

Lionel Messi
Lionel Messi AFP PHOTO / PABLO PORCIUNCULA

Baada ya kumalizika kwa kesi yake hapo kesho, Messi atahabiri ndege kuelekea nchini Marekani ambako timu yake ya taifa ya Argentina inashiriki kwenye michuano ya Copa Amerika ambapo itacheza na mabingwa watetezi wa kombe hilo, Chile, siku ya Jumatatu.

Kesi hii iliyovuta hisia kubwa duniani, ilianza kung'oa nanga bila ya Messi mwenyewe kuwepo mahakamani siku ya Jumatatu, kwakuwa alikuwa bado yuko nchini mwake akiendelea kupatiwa matibabu ya uti wa mgongo baada ya kupata majeraha kwenye mechi yao ya kirafiki dhidi ya Honduras.

Chini ya sheria za Uhispania, mtuhumiwa halazimishwi kuhudhuria vikao vyote vya kesi yake ikiwa mwendesha mashtaka anaiomba mahakama imuhukumu kifungo cha chini ya miaka miwili.

Mshauri wa zamani wa masuala ya kodi wa Lionel Messi, amemuunga mkono mteja wake wakati alipopanda kizimbani, akidai kuwa mchezaji huyo hana ufahamu wowote kuhusu mwenendo wake wa masuala ya fedha kwakuwa anayeshughulikia ni baba yake.

Mchezaji huyo wa Barcelona pamoja na mawakili wake, wameendelea kusisitiza kuwa baba yake ndiye anayehusika na masuala yote ya kifedha yanayomuhusu mchezaji huyo, na kwamba hakuwa na usemi wowote.

Mwendesha mashtaka wa Uhispania anaiomba mahakama imuhukumu Messi pamoja na baba yake kifungo cha miezi 22 jela ikiwa watapatikana na hatia sambamba na kulipa fidia yenye thamani sawa na kiwango walichodaiwa kukwepa kulipa kodi.

Wataalamu wa sheria wanaona kuwa huenda mchezaji huyo na baba yake wasihukumiwe kwa namna mfumo wa sheria wa Uhispania unavyofanya kazi kwa watu wanaopatikana na kosa la kwanza, ambapo pia mwaka 2013, baada ya kuanzishwa uchunguzi dhidi yao, walilipa kiasi cha dola za Marekani milioni 5.6 kama sehemu ya kodi waliydaiwa kukwepa kuilipa.