SOKA

AFCON 2017: Kenya yadidimiza matumaini ya Congo Brazaville kufuzu

Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars.
Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars. youtube

Matumaini ya timu ya taifa ya Congo Brazaville kufuzu kucheza fainali ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka ujao nchini Gabon, yamezimwa na Kenya baada ya kufungwa mabao 2 kwa 1 jijini Nairobi Jumapili jioni.

Matangazo ya kibiashara

Matokeo haya yanaipa Guinea Bissau nafasi ya kipekee kufuzu katika michuano hii kwa mara ya kwanza katika historia yake ya soka baada ya kupata ushindi muhimu jana wa mabao 3 kwa 2 dhidi ya Zambia mjini Bissau.

Congo Brazaville ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia mkwaju wa penalti uliotiwa wavuni na Prince Oniangue, dakika ya 19 ya mchezo huo lakini dakika 5 baadaye, Ayub Timbe akaisawazishia Harambee Stars katika dakika ya 24 baada ya kuwachenga mabeki wa Congo Brazaville na kutikisa nyavu.

Kenya ilitawala mchezo huo katika vipindi vyote na licha ya kukosa nafasi nyingi za kufunga, hatimaye Johanna Omollo aliifungia timu yake bao la pili na la ushindi katika dakika 67, baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa nahodha wake Victor Wanyama na kufunga kwa mkwaju wa juu uliomshinda kipa wa Congo Brazaville.

Wachezaji wa Kenya  na Congo Brazaville wakipambana
Wachezaji wa Kenya na Congo Brazaville wakipambana

Huu ndio ushindi wa kwanza wa kocha Stanley Okumbi ambaye amekuwa akikosolewa na mashabiki wa soka nchini Kenya, kwa madai kuwa hana uwezo wa kuifunza timu ya taifa tangu kuchaguliwa kwake mwezi Machi mwaka huu.

Mchezo wa mwisho wa Kenya utakuwa dhidi ya Zambia mwezi Septemba mjini Ndola, huku Congo wakiwakaribisha Guinea Bissau.

Kwa matokeo haya ya Jumapili, Guinea Bissau wanaongoza kundi la E kwa alama 10, wakifuatwa na Congo ambao wana alama 6 na hata wakishinda mechi inayosalia hawawezi kufikia alama zaidi ya 10.

Zambia inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 6, huku Kenya ikiwa ya mwisho mwa alama 4.

Matokeo mengine siku ya Jumapili:-

Mauritius 0 Ghana 2
Madagascar 1 DR Congo 6
Comoros 0 Burkina Faso 1