EURO 2016

Mashabiki wa 'Le Bleus' wapiga picha na wachezaji wao kuelekea mechi na Romania

Wachezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa wakifanya mazoezi
Wachezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa wakifanya mazoezi REUTERS/Vincent Kessler

Mashabiki wa timu ya taifa ya Ufaransa, juma hili walipata zawadi ya aina yake wakati walipohudhuria mazoezi ya timu yao kwenye eneo la Clairefontaine, ambapo wachezaji wa timu hiyo walisaini mashati na vifaa mbalimbali vya mashabiki sambamba na kupiga picha na mashabiki waliohudhuria mazoezi ya mwisho ya ya wazi ya timu hiyo. 

Matangazo ya kibiashara

Nahodha wa timu hiyo, mlinda mlango Hugo Lloris, aliongoza wachezaji wenzake kuelekea kwenye jukwaa lililokuwa na maelfu ya mashabiki, ambao walisainiwa vitu walivyokuja navyo, huku wachezaji Antoine Griezmann, Olivier Giroud na Blaise Matuidi wakiwa miongoni mwa waliowavutia wachezaji.

Wakati wa mazoezi ya timu hiyo, mashambuliaji wa klabu ya Atletico Madrid, Griezmann, ambaye alicheza fainali ya mwaka huu ya michuano ya klabu bingwa Ulaya na ambaye wachambuzi wanaona kuwa ndiye mchezaji pekee atakayeanza kwenye kikosi kitakachocheza mechi ya ufunguzi ijumaa hii dhidi ya Romania.

Miongoni mwa wachezaji wengine wanaopewa nafasi ya kuanza kwenye mchezo wa Ijumaa ni pamoja na kiungo mkabaji wa Juventus ya Italia, Paul Pogba, ambaye alikuwa akifanya mazoezi ya kucheza na mpira.

Baada ya kumalizika kwa mazoezi ya kwanza, wachezaji wa "Le Bleus" walielekea kwenye jukwaa walilokuwepo mashabiki ambao walikuwa wanawasubiri mashujaa wao tayari kupiga nao picha.