EURO 2016

Hofu ya usalama yatanda, kombe la Ulaya likianza leo

Eneo la mnara wa Tour Eiffel ambalo ni maarufu jiji Paris
Eneo la mnara wa Tour Eiffel ambalo ni maarufu jiji Paris REUTERS/Charles Platiau

Michuano ya mpira wa miguu, kombe la mataifa Ulaya, inaanza hili leo nchini Ufaransa, huku kukiwa na hofu kubwa ya kiusalama, wakati huu rais Francois Hollande akiapa kuchukua hatua madhubuti kuzuia jaribio lolote linalonga kuharibu sura ya michuano hii. 

Matangazo ya kibiashara

Michuano hii inaanza kwa timu ya taifa ya Ufaransa ambayo ndiyo mwenyeji kucheza na timu ya taifa ya Romania, mtanange utakaopigwa kwenye dimba la "Stade de France" jijini Paris, maajira ya saa nne kamili za usiku kwa saa za hapa Afrika ya Kati.

Mechi hii ya ufunguzi inachezwa wakati huu taifa la Ufaransa likikabiliwa na maandamano ya wafanyakazi nchi nzima wanaoshinikiza mabadiliko ya sheria ya kazi, sambamba na kitisho cha ugaidi kulenga viwanja na maeneo ambayo mashabiki watakuwa.

Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps akiwa na mwenzake Guy Stéphan wakitazama mazoezi ya timu yao
Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps akiwa na mwenzake Guy Stéphan wakitazama mazoezi ya timu yao RFI/Pierre René-Worms

Mifuko na makasha mengine ya uchafu yaliokotwa kwenye viunga mbalimbali vya jiji la Paris, ambako mechi ya ufunguzi itafanyika, huku shirikisho la wafanyakazi wa sekta ya usafiri nchini humo likitishia kufanya maandamano makubwa.

Kwenye hotuba yake rais Hollande amesema kwamba Serikali yake haitaketi na kutazama baadhi ya watu wachache wakitatiza hali ya usalama wakati huu wa michuano ya Ulaya.

Rais Hollande ameongeza kuwa tayari hatua madhubuti na muhimu zimeshachukuliwa kuhakikisha michuano ya mwaka huu inayofanyika nchini mwake inafanyika kwa amani na utulivu bila bugudha.

Zaidi ya askari na wanajeshi elfu tisini wale wa uma na binafsi wamesambazwa kwenye maeneo mbalimbali ya nchi kwaajili ya kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wote wa michuano hii.

Wachezaji wa Ufaransa wakiwa wamepumzika baada ya mazoezi, leo wanacheza na Romania
Wachezaji wa Ufaransa wakiwa wamepumzika baada ya mazoezi, leo wanacheza na Romania RFI/Pierre René-Worms

Hali ya usalama kuimarishwa na namna itakavyokuwa, ilishuhudiwa wakati mwanamuziki maarufu nchini humo DJ David Guetta alipofanya tamasha kubwa la muziki jijini Paris bila ya kujitokeza tukio lolote lililohatarisha usalama.

Mamia kwa maelfu ya mashabiki wameanza kufurika jijini Paris tayari kuanza kushuhudia michuano ya mwaka huu, huku tishio la mgomo wa madereva wa treni na mabasi unahofiwa utatatiza shughuli za usafiri wakati wa michuano hii.

Waziri wa mazingira, Segolene Royal, ametoa wito kwa viongozi wa mashirikisho ya wafanyakazi nchini humo kutoharibu taswira ya michuano ya Euro, na kwamba kufanya mgomo kutaharibu sura ya taifa lao na hata uwezekano wa kuzawadiwa zabuni ya kuandaa michuano ya Olympic ya mwaka 2024 ambayo Ufaransa inataka kuandaa.