EURO 2016

Euro 2016: Mechi za wikiendi kuendelea, usalama waimarishwa

Shabiki wa timu ya taifa ya Albania kabla ya mechi dhidi ya Uswis
Shabiki wa timu ya taifa ya Albania kabla ya mechi dhidi ya Uswis REUTERS/John Sibley Livepic

Baada ya wenye timu ya taifa Ufaransa kuanza vyema michuano ya kombe la Ulaya, leo ni zamu ya Albania, Uswis, Wales, Slovakia, Uingereza na Urusi.

Matangazo ya kibiashara

Timu ya taifa ya Albania yenyewe itakuwa uwanjani kucheza na Uswis katika mchezo wa kundi A, ambapo hapo jana wenyeji Ufaransa walianza vyema baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Romania, shukrani kwa mabao ya Giroud na Payet aliyefunga kwenye dakika za lala salama.

Kundi B pia kutakuwa na mechi Juni 11, Jumamosi, ambapo timu ya taifa ya Wales watawakaribisha Slovakia, kwenye mchezo ambao watu wengi wanaipa nafasi Wales kuibuka na ushindi ingawa mpira ni dakika 90, kwakuwa Slovakia nao sio timu ya kubeza.

Antoine Griezmann wa Ufaransa na Alexandru Chipciu wa Romania
Antoine Griezmann wa Ufaransa na Alexandru Chipciu wa Romania Franck FIFE Daniel MIHAILESCU / AFP

Mchezo mwingine wa kundi B, utakuwa ni ule utakaozikutanisha timu ya taifa ya Uingereza ambayo itacheza na timu ya taifa ya Urusi, kwenye mchezo ambao unazikutanisha timu ambazo sio tu ni mahasimu kwenye kabumbu, lakini hata kwenye masuala ya siasa na uchumi.

Mechi kati ya Albania na Uswis itapigwa saa kumi kamili kwa saa za Afrika Mashariki, huku, ile ya Wales dhidi ya Slovakia itapigwa saa moja kamili kwa saa za Afrika Mashariki, huku ile ya Uingereza na Urusi, ikitarajiwa kupigwa saa nne kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Uingereza wakiendelea na mazoezi kabla ya mechi yao na Urusi
Wachezaji wa timu ya taifa ya Uingereza wakiendelea na mazoezi kabla ya mechi yao na Urusi REUTERS/Lee Smith

Katika hatua nyingine, wakati michuano hii ikiwa imeanza kwa kufana hapo jana, huenda yakatiwa dosari, baada ya wafanyakazi wa shirika la ndege la uma nchini Ufaransa, kutangaza kuanza mgomo wao wa siku nne.

Wafanyakazi wa Air France wamesema safari za maeneo mengine nje ya taifa hilo zitaendelea kama kawaida lakini wamesitisha safari za kwenye miji ambayo fainali hizi zinafanyika, hatua ambayo huenda ikaathiri mashabiki wengi wa soka waliokuwa wamepanga kutumia shirika hilo la ndege.

Usalama umeendelea kuimarishwa kwenye maeneo mengi ya nchi, kufuatia kuwepo kwa tishio la kutekelezwa mashambulizi ya kigaidi, ambapo polisi na wanajeshi wamekuwa wakiwakagua watu kwa kina ili kuzuia kujitokeza kwa tukio lolote linaloweza kutatiza usalama.

Katika hatua nyingine, kadi ya kwanza nyekundu kwenye michuano ya Ulaya, imetolewa kwa mchezaji wa timu ya taifa ya Albania, Lorik Cana, baada ya kuushika kwa makusudi mpira jirani na eneo lake la hatari.