EURO 2016

Uswis yaanza vema mechi za kombe la Ulaya 2016

Mchezaji wa Uswis, Fabian Schar akiifungia timu yake bao la kwanza dhidi ya Albania, tarehe 11 Juni 2016, kombe la Ulaya 2016
Mchezaji wa Uswis, Fabian Schar akiifungia timu yake bao la kwanza dhidi ya Albania, tarehe 11 Juni 2016, kombe la Ulaya 2016 REUTERS/Carl Recine Livepic

Timu ya taifa ya Uswis imeanza vyema michuano ya kombe la Ulaya 2016, baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Albania kwa bao 1-0, kwenye mchezo uliopigwa kwenye dimba la Bollaert-Delelis, mjini Lens.

Matangazo ya kibiashara

Uswis iliingia kwenye mchezo huu uliopigwa Jumamosi, Juni 11 ikiwa na matumaini ya kuanza vyema kutupa karata yake ya kwanza kwenye mchezo wa kundi A, ambapo ilifanikiwa kukipata kile ilichoingia nacho uwanjani.

Albania licha ya kuonesha upinzani mkali haikufanikiwa kufua dafu mbele ya Uswis kwani mara kadhaa licha ya kupata nafasi za kusawazisha bao, washambuliaji wake hawakuwa makini kufunga.

Uswis na wao itabidi wajilaumu kwa kukosa mabao mengi kwenye kipindi cha kwanza, mabao ambayo pengine yangetosha kuipatia ushindi mnono kwenye mecho yao ya kwanza.

Uswis ilipata bao lake la kwanza kwenye dakika ya 5 ya mchezo kupitia kwa Fabian Schar, ambaye aliwazidi ujanja mabeki na kipa wa Albania aliyechelewa kutokea kuuokoa mpira wa krosi.

Uswis sasa inalingana alama na Ufaransa wenyeji wa michuano hii kwa kuwa na alama tatu kila mmoja lakini wametofautiana magoli ya kufunga.