EURO 2016

UEFA yatishia kuziondoa Urusi na Uingereza

Vurugu kati ya mashabiki wa Urusi na Uingereza
Vurugu kati ya mashabiki wa Urusi na Uingereza REUTERS/Jean-Paul Pelissier

Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limetishia kuziondoa Uingereza na Urusi katika michuano inayoendelea ya soka nchini Ufaransa kuwania taji la bara Ulaya ikiwa mashabiki wa nchi hizo mbili watashiriki tena katika vurugu kama ilivyoshuhudiwa siku ya Jumamosi.

Matangazo ya kibiashara

UEFA imesisitiza kuwa pamoja na onyo hilo imeanza uchunguzi wa kina dhidi ya Urusi ambayo mashabiki wake walianza kuwavamia wale wa Uingereza, baada ya mchuano kati ya nchi hizo mbili kumalizika kwa sare ya bao 1 kwa 1 mjini Marseille.

Serikali ya Uingereza imesema iko tayari kuongeza nguvu kwa kutuma polisi wake kusaidia kuwadhibiti mashabiki wa nchi yake wakati wa mchuano wao wa pili wiki ijayo.

Shabiki wa Urusi
Shabiki wa Urusi REUTERS/Jean-Paul Pelissier

Mashabiki wa Urusi wanashtumiwa kuanza vurugu baada ya kurusha fataki kwa mashabiki wa Uingereza wakati mchuano huo ukikaribia kufika mwisho na kusababisha makabiliano zaidi.

UEFA inasema itaichukua Urusi hatua baada ya mashabiki wake kuzua fujo, kuonesha vitendo vya ubaguzi wa rangi na kutumia fataki kuwashambulia mashabiki wa Uingereza.

Waziri wa Michezo wa Urusi Vitaly Mutko amenukulia akisema anaunga mkono uchunguzi wa UEFA na kusisitiza kuwa tabia ya mashabiki wa nchi yake haikubaliki katika mchezo wa soka.