COPA AMERIKA

Brazil yatupwa nje hatua ya makundi, Copa Amerika

Wachezaji wa timu ya taifa ya Brazil wanaoshiriki michuano ya Copa Amerika
Wachezaji wa timu ya taifa ya Brazil wanaoshiriki michuano ya Copa Amerika REUTERS

Mabingwa mara tano wa kombe la dunia, timu ya taifa ya Brazil, imepoteza mchezo wake wa hatua ya makundi kwenye michuano ya Copa Amerika dhidi ya Peru, na kuondolewa kwenye hatua hiyo ya makundi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30, baada ya kufungwa bao 1-0.

Matangazo ya kibiashara

Timu ya taifa ya Brazil ilikuwa haijawi kufungwa na Peru katika michezo 16 iliyopita na ambayo waliwahi kukutana, na walikuwa wanahitaji kupata alama moja tu ili wafuzu kwenye hatua ya robo fainali.

Mchezaji aliyeingia kipindi cha pili, Raul Ruidiaz, aliipatia timu yake bao la kuongoza na la ushindi katika dakika ya 75 ya mchezo ambapo Brazil imelalama kuwa mpira ulimgonga mkononi mfungaji kabla ya kufunga.

Ecuador wao waliwafunga Haiti kwa mabao 4-0 na kufuzu kwenye hatua ya robo fainali iki ni mara ya kwanza toka walipofanya hivyo mwaka 1997.

Brazil ilishindwa kuifunga timu ya taifa ya Peru wala Ecuador mara zote ilipokutana nazo, licha ya kupata ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya timu ya taifa ya Haiti.

Akiulizwa na wanahabari kuhusu hatma yake kama kocha wa Brazil, kocha mkuu wa timu hiyo na mchezaji wa zamani, Dunga, amesema yeye anaogopa kifo tu na haogopi kuhusu nafasi yake kama kocha.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Brazil walimzonga mwamuzi raia wa Uruguay, Andres Cunha, lakini baada ya mwamuzi huyo kuzungumza na mwamuzi wa mezani, aliamua kusalia na uamuzi wake na kulikubali goli.