EURO 2016

Ujerumani yaanza vema mechi za kombe la Ulaya 2016

Mabingwa wa dunia, timu ya taifa ya Ujerumani, imeanza vema michuano ya kombe la Ulaya nchini Ufaransa, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa bila dhidi ya timu ya taifa ya Ukraine. 

Kiungo wa Ujerumani ambaye alikuwa mchezaji bora wa mchezo, Toni Kroos, kombe la Ulaya 2016
Kiungo wa Ujerumani ambaye alikuwa mchezaji bora wa mchezo, Toni Kroos, kombe la Ulaya 2016 REUTERS/Pascal Rossignol Livepic
Matangazo ya kibiashara

Ushindi huu wa Ujerumani, unaweka hai matumaini yake ya kufanikiwa kutwaa taji la nne la michuano hii ya Ulaya, ambapo matarajio makubwa kwa timu hii ni kuona inafika hatua ya fainali.

Licha ya kiwango kizuri kilichooneshwa na kiungo, Toni Kroos na bao la mapema lililofingwa na Shkodran Mustafi, timu hiyo bado ilijikuta kwenye wakati mgumu kutoka kwa washambuliaji wa Ukraine, ambao lazima wajilaumu wenyewe kwa kukosa magoli ya wazi.

Beki wake wa kati, Jerome Boateng, aliiokoa Ujerumani isufungwe bao la mapema, baada ya kuuondoa mpira uliokuwa unaingia golini ambapo mlinda mlango Manuel Neuer alikuwa tayari ameelekea markiti.

REUTERS/Eric Gaillard Livepic

Shukrani pia zitamuendea mlinda mlango wa Ujerumani, Manuel Neuer, ambaye kwa sehemu kubwa ya mchezo, aliokoa michomo ya wazi ambayo ingeweza kuwapa wakati mgumu dhidi ya wapinzani wao.

Hata hivyo ndoto za Ukraine kupata bao la kusawazisha zilizimwa kabisa na kiungo wa kimataifa na mkongwe, aliyeingia kipindi cha pili, Bastian Schweinsteiger, ambaye baada ya kuingia tu akaipatia timu yake bao la pili na la ushindi.

Baada ya timu ya taifa ya Polans kuibuka na ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Ireland Kaskazini siku ya Jumapili, Ujerumani sasa itakuwa inaongoza kwenye kundi C, ambapo Alhamisi watacheza na Poland, ambao waliwafunga wakati wa mechi za kufuzu kucheza fainali za mwaka huu.