EURO 2016

FA yahofia usalama wa mashabiki wake Lille

Mashabiki wa Urusi na wale wa Uingereza wakikabiliana mara baada ya timu zao kumaliza kucheza
Mashabiki wa Urusi na wale wa Uingereza wakikabiliana mara baada ya timu zao kumaliza kucheza REUTERS/Kai Pfaffenbach Livepic

Shirikisho la soka nchini Uingereza, FA, limeeleza kuguswa na hali ya usalama itakavyokuwa kwenye mji wa Lille, ambako mashabiki wa Uingereza na wale wa Urusi wanatarajiwa kuwa pamoja kwenye mji huo mwishoni mwa juma kwaajili ya mechi za kombe la Ulaya, amesema Greg Dyke, rais wa FA.

Matangazo ya kibiashara

Mashabiki wa timu ya Uingereza wanatarajiwa kuwa mjini Lille kushuhudia timu yao itakaposhuka dimbani Alhamisi ya wiki hii kuwakabili mahasimu wao timu ya taifa ya Wales, mji jirani kabisa na Lens ambako mashabiki wa Urusi watakuwa huko kushuhudia timu yao ikicheza na Slovakia siku ya Jumatano.

Mwendesha mashtaka wa Serikali ya Ufaransa, amesema kuwa zaidi ya mashabiki 150 wa Urusi na ambao hawajapatikana mpaka sasa, walihusika kwa asilimia mia moja na vurugu za mwishoni mwa juma lililopita.

Mashabiki sita wa Uingereza wamehukumiwa kwenda jela baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika kwenye vurugu za siku ya Jumamosi, hukumu ambayo hata hivyo imekosolewa na wazazi wao.

Mashabiki wengine wawili wa Urusi, wao walikamatwa kwa kosa la kuvamia na kuingia uwanjani mara baada ya mchezo.

Timu zote mbili huenda zikaondolewa kwenye michuano ya mwaka huu na shirikisho la mpira Ulaya, UEFA ambao ndio waandaaji, ikiwa mashabiki hao watajihusisha na vurugu nyingine.

Kwenye barua yake kwa shirikisho la mpira Ulaya, UEFA, rais wa FA, amekanusha vikali tuhuma kwamba mashabiki wake ndio waliosababisha vurugu zilizoshuhudiwa siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Stade Velodrone.

FA badala yake inaitaka UEFA na Polisi nchini Ufaransa kushirikiana na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wahusika wakuu wa vurugu za mwishoni mwa juma wanakamatwa na kushtakiwa.