BRAZILI - DUNGA

Dunga afutwa kazi, mrithi wake aanza kutafutwa

Aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil, Dunga
Aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil, Dunga REUTERS/Ricardo Moraes

Shirikisho la mpira wa miguu nchini Brazil, limetangaza kumfuta kazi kocha mkuu wa timu ya taifa, Dunga, siku chache baada ya timu hiyo kuondolewa kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Copa Amerika. 

Matangazo ya kibiashara

Dunga, ambaye aliiongoza Brazil kushinda taji la kombe la dunia mwaka 1994, alipewa jukumu hili la kukinoa kikosi cha Brazil kwa mara ya pili mwaka 2014.

Licha ya matarajio makubwa iliyokuwa nayo timu hiyo, waliduwazwa baada ya kuondolewa mapema tu kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Copa Amerika, ikiwa ni mara ya kwanza toka mwaka 1987 baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Peru, mjini Massachussetts.

Dunga, wakati fulani akiwa kocha wa timu hiyo kati ya mwaka 2006 na 2010, aliisaidia timu yake kutwaa taji la michuano ya Copa Amerika, mwaka 2007.

Kocha wa klabu wa Corinthians, Tite anapewa nafasi kubwa ya kuchukua mikoba ya Dunga.

Tite aliiongoza klabu yake kuchukua ubingwa wa ligi ya Brazili Seria A mwaka 2011 na 2015, sambamba na kombe la Copa Libertadores na lile la dunia kwa upande wa vilabu mwaka 2012.

Kwa yeyote yule atakayerithi mikoba ya Dunga, atatakiwa kukiongoza kikosi cha taifa cha Brazil cha wachezaji walio na umri wa chini ya miaka 23, kitakachomjumuisha pia mchambuliaji wa Barcelona, Neymar, wakati wa michuano ya Olympic itakayofanyika jijini Rio de Janeiro.

Mrithi wa Dunga pia atakuwa na jukumu la kuiongoza Brazil kufuzu kucheza kombe la dunia la mwaka 2018 nchini Urusi, ambapo tayari imeanza vibaya na inashika nafasi ya 6 kwenye nchi za Amerika Kusini.