EURO 2016

Hungary, Iceland zawaduwaza mashabiki wa soka

Mchezaji wa Hungary, Zoltan Stieber, akiifungia timu yake bao la 2 na laushindi dhidi ya Austria.
Mchezaji wa Hungary, Zoltan Stieber, akiifungia timu yake bao la 2 na laushindi dhidi ya Austria. REUTERS/Sergio Perez Livepic

Timu ya taifa ya Iceland imefanikiwa kupata alama moja ambayo timu hiyo itaikumbuka kwenye mashindano ya mwaka huu ya kombe la Ulaya ambayo ni mara yake ya kwanza kushiriki, baada ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Ureno kwenye mchezo wa kundi F. 

Matangazo ya kibiashara

Kipindi cha kwanza mchezaji wa Iceland, Gylfi Sigurdsson almanusura aipatie timu yake bao la kuongoza katika dakika za mwanzo tu za mchezo, lakini akajikuta shuti lake likiokolewa na mlinda mlango wa Ureno.

Lakini wakati Iceland wakiwa wanajipanga kupata bao la kuongeza winga wa Ureno, Luis Nani aliiandikia Ureno bao la kuongoza, bao ambao hata hivyo halikudumu sana kwani mchezaji Birkir Bjarnason aliwashangaza Ureno kwa kusawazisha baso safi.

Mashambulizi kwa pande zote mbili yaliongezeka ambapo kichwa cha Christian Ronaldo kiliokolewa na mlinda mlango wa Iceland, kabla ya Alfred Finngogason nae kuachia shuti lililookolewa na mlinda mlango wa Ureno.

Mchezaji wa Iceland, Birkir Bjarnason akishangilia baada ya kuifungia timu yake goli.
Mchezaji wa Iceland, Birkir Bjarnason akishangilia baada ya kuifungia timu yake goli. REUTERS/Kai Pfaffenbach Livepic

Kwenye mchezo mwingine timu ya taifa ya Hungary, ilipata matokeo yaliyowashangaza wengi, baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mahasimu wao wa siku nyingi waliojitenga, Austria.

Sekunde ya 28 punde baada ya mchezi huo kuanza almanusura Austria wapate bao la kuongoza, baada ya mchezaji wake David Alaba kuachia fataki lililogonga mwamba wa goli na kurejea uwanjani.

Hungary baada ya kukoswakoswa walitulia na kuanza kuwasoma wapinzani wao ambapo haikuchukua muda kabla ya timu hiyo kupata bao la kuongoza kupitia kwa Adam Szalai akiunganisha pasi ya Laszlo Kleinheiser.

Austria walijikuta wakicheza pungufu baada ya mchezaji wake Aleksandar Dragovic kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi, ambapo dakika chache baadae bao la Zoltan Stieber lilihitimisha sherehe za Hungary.