ICGLR - USALAMA

ICGLR: Changamoto za usalama bado ni kubwa

Wakuu wa nchi za maziwa mkuu, walipokutana mjini Angola, kuanzia Jumanne, 14 June 2016
Wakuu wa nchi za maziwa mkuu, walipokutana mjini Angola, kuanzia Jumanne, 14 June 2016 Kenya Govt

Wakuu wa nchi za Jumuiya ya nchi za maziwa makuu, wamemaliza mkutano wao mjini Luanda, Angola na kukubaliana kuanza utekelezwaji wa masuala kadhaa hasa ya kiusalama kwenye nchi zenye migogoro. 

Matangazo ya kibiashara

Wakuu hao wa nchi wamesisitiza umuhimu wa jukumu lao la kwanza la kuhakikisha wanapata suluhu na kushughulikia changamoto za kiusalama kwenye nchi wanachama, wakiapa kutekeleza itifaki ya jumuiya hiyo kuhusu usalama.

Kwenye mkutano huo, wakuu hao wa nchi wamempongeza katibu mkuu wa jumuiya anayemaliza muda wake Profesa Ntumba Luaba, kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa muda wote akiwa katibu mkuu wa ICGLR.

Miongoni mwa masuala ambayo viongozi hawa wamekubaliana na kuagiza yafanyike ni pamoja na :

Kuiagiza kamati maalumu ya kufanya tathmini kwenye nchi za ukanda, EJVM, kufanya uhakiki na kueleza kinagaubaga sababu na malengo ya kukamatwa kwa raia wanaodaiwa kuwa ni kutoka Burundi wanaoshikiliwa na Serikali ya DRC, na kutoa ripoti yao ndani ya siku 60.

Viongozi wa nchi za maziwa makuu wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumaliza mkutano wao, mjini Luanda, Angola.
Viongozi wa nchi za maziwa makuu wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumaliza mkutano wao, mjini Luanda, Angola. Kenya Govt

Wakuu hao pia wamekaribisha kuanza upya kwa mazungumzo ya amani kuhusu Burundi, yanayoratibiwa na rais wa zamani wa Tanzania, Benjamini William Mkapa, na kutoa wito kwa Serikali na upinzani kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa kupata amani nchini humo.

Wakuu hao pia wamekubaliana na kuona umuhimu wa vikao vyao vijavyo, kumualika mratibu wa mazungumzo ya Burundi, rais Mkapa, ili aeleze hatua ambazo anakuwa amezifikia na kutoa mapendekezo ili ICGLR isaidie pale panapohitajika.

Pia wakuu hao wa nchi wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuisaidia kifedha nchi ya Burundi na kuongeza misaada kwa mamia ya wakimbizi wa Burundi waliokimbilia nchi jirani.

Mkutano huo pia umepongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali ya DRC, katika harakati zake za kutokomeza makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo, hasa makundi ya ADF na FDLR, kwa kushirikiana na vikosi vya Serikali FARDC na vile vya umoja wa Mataifa, MONUSCO.

Kikao hiki pia kimeunga mkono makubaliano ya wakuu wa nchi za Uganda, Kenya, Tanzania na DRC, kufanya tathmini ya athari za kuenea kwa itikadi za kiislamu, zinazoenezwa na kundi la ADF.

Wakuu hao pia wamepongeza mchakato wa kusaka muafaka wa hali ya siasa nchini DRC ili nchi hiyo iweze kuandaa uchaguzi ulio huru na haki kama ilivyoelekezwa kwenye katiba ya nchi.

Suala jingine walilopendekeza ni pamoja na kuundwa kwa kamati maalumu ya nchi wanachama za ICGLR, itakayokuwa na jukumu la kupitia na kutathmini hali ya usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, pamoja na kulimaliza kabisa kundi la LRA linalotishia usalama wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Viongozi hao pia, wamewapongeza wakuu wa nchi ya Sudan Kusini kwa kufikia makubaliano na kuanza kutekeleza mkataba wa amani walioutia saini mwezi August mwaka jana ambapo umepelekea kuundwa kwa Serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa.