EURO 2016

Ulinzi waimarishwa Lille kudhibiti vurugu za mashabiki

Mashabiki wa Uingereza wakiwa wamewasha fataki kuwakabili Polisi wa Ufaransa, 15 June 2016
Mashabiki wa Uingereza wakiwa wamewasha fataki kuwakabili Polisi wa Ufaransa, 15 June 2016 REUTERS/Christian Hartmann

Watu zaidi ya 36 wanashikiliwa na vyombo vya usalama nchini Ufaransa kwenye mji wa Lille, baada ya kutokea makabiliano kati ya Polisi wa kutuliza ghasia na mashabiki wa michuano ya kombe la Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Polisi nchini Ufaransa inasema kuwa operesheni ya kuwakamata mashabiki wa soka wanaojihusisha na vurugu wakati wa michuano ya mwaka huu imeendelea usiku kucha hadi kuamkia hivi leo, ambapo watu wengine 16 wamejeruhiwa.

Jumatano jioni, Polisi wa kutuliza ghasia waliwakabili mashabiki wa soka wa Uingereza waliokuwa wamewasha miale na fataki, wakati walipojaribu kukabiliana na mashabiki wa Urusi.

Taarifa ya Polisi kwenye mji wa Lille zinasema kuwa mashabiki wengi waliokamatwa ni wale mashabiki wa timu ya taifa ya Uingereza, ambao kwa sehemu kubwa ndio wanadaiwa kuhusika kwenye vurugu.

Awali kabla ya makabiliano hayo, mashabiki kadhaa wa Urusi na wale wa Uingereza walikamatwa na Polisi baada ya mashabiki hao kuanza kukabiliana kwa mara nyingine, licha ya onyo lililotolewa na shirikisho la mpira Ulaya, Uefa.

Mashabiki wa Uingereza wakitawanywa kwa kutumia mabomu ya machozi mjini Lille, 15 June 2016
Mashabiki wa Uingereza wakitawanywa kwa kutumia mabomu ya machozi mjini Lille, 15 June 2016 REUTERS/Wolfgang Rattay

Kumekuwa na hofu ya kutokea vurugu kwenye mji wa Lille, ambapo hii leo timu ya taifa ya Uingereza itakuwa inawakabili majirani na mahasimu wao kwenye kabumbu timu ya taifa ya Wales.

Ulinzi mkali umewekwa kwenye maeneo mengi ya mji wa Lille, ambako mechi hiyo itachezwa, huku mashabiki wa Urusi wakitakiwa kuondoka kwenye maeneo ambayo,mashabiki wa Uingereza watakuwepo kuepusha machafuko zaidi.

Katika hatua nyingine, Utawala wa Moscow alimuita balozi wa Ufaransa nchini humo na kumtaka atoe maelezo kuhusu operesheni inayoendelea ya kuwakamata mashabiki wa timu yao.

Wakati huu Polisi ikiendelea kuwakamata mashabiki zaidi, hapo jana maofisa usalama walitangaza kuwafikisha mahakamani mashabiki sita zaidi ya Urusi, huku wengine zaidi ya watatu mashabiki wa Urusi na Ukraine, wakitarajiwa kurejeshwa nchini mwao.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema kuwa kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa mashabiki wa timu yao, ni suala ambao halikubaliki na kuonya kuhusu uwezekano wa kutatizika kwa uhusiano baina ya nchi hizo mbili.