URUSI - WADA

Wada: Maofisa wetu Urusi wamepokea vitisho

Wataalamu wa maabara kwenye kutio cha wada nchini Urusi, wakifanyia majaribio sampuli mpya
Wataalamu wa maabara kwenye kutio cha wada nchini Urusi, wakifanyia majaribio sampuli mpya REUTERS/Sergei Karpukhin

Maofisa nchini Urusi wanaofanya vipimo kwa wanamichezo kubaini ikiwa wanatumia dawa za kusisimua misuli au la, wanazuiwa kutimiza majukumu yao pamoja na kupokea vitisho kutoka kwa vyombo vya usalama, ripoti mpya imeonesha.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la dunia linalopinga matumizi ya dawa zinazokatazwa michezoni, Wada, limetoa ripoti yake mpya ikiwa ni siku mbili tu kabla ya Urusi kufahamu hatma yake ikiwa itatuma wanamichezo wake kushiriki mashindano Olympic ya jijini Rio.

Wanamichezo wa Urusi walikuwa wamefungiwa kushiriki mashindano yoyote ya kimataifa baada ya Wada, kuituhumu Urusi kushiriki kwenye mpango wa kuficha na kusaidia wanamichezo wake kukwepa kupimwa damu kubaini ikiwa walitumia dawa zilizokatazwa michezoni.

Wakuu wa shirika hilo wanakutana Ijumaa ya wiki hii, kuamua ikiwa waiondolee Urusi adhabu hiyo au la, uamuzi ambao unasubiriwa kwa hamu na wanamichezo wa Urusi wanaotarajiwa kushiriki mashindano ya Olympic.

REUTERS/Christinne Muschi

Wada inasema kuwa: Sampuli 73 kati ya 455 za wanamichezo wa Urusi hazikuchukuliwa, sampuli 736 zilikataliwa na zilifutwa, sampuli 23 zilipoteza na ambazo ripoti inasema zilikuwa ni idadi kubwa huku sampuli 52 zikionesha kuwa chanya.

Ripoti ya Wada imeonesha kwa kina namna wanariadha kutoka kwenye michezo mbalimbali walivyokwepa na kulidanganya shirika linalopima wanamichezo ikiwa wametumia dawa za kusisimua misuli au la.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa mmoja wa wanariadha alionekana kukimbia kutoka kwenye mstari wa wanamichezo waliotakiwa kupimwa, huku mwingine akitoweka kwenye mazingira ya kutatanisha baada ya kumaliza mbio.

Wada inasema kuwa wanamichezo wengi wa Urusi, walitumia vichupa ambavyo havikuwa salama, kwa lengo la kuharibu uchunguzi wa sampuli za mkojo.

Ripoti imeongeza kuwa baada ya wanamichezo walienda mbali zaidi na hata kudiriki kuwahonga maofisa wa shirika la DCO la nchini Urusi ambalo linawapima wanamichezo, ili vipimo vyao vioneshe kuwa hawakutumia dawa zozote zilizokatazwa.

Ripoti hii mpya ya Wada inasema kuwa maofisa wa DCO wamekuwa wakitishiwa wakati wanapojaribu kutembelea vituo vya kijeshi na kutishiwa na vilipuzi kutoka kwa wanajeshi, kwamba baadhi ya sampuli zilizopelekwa kwa wawakilishi wa Wada zilifikishwa zikiwa tayari zimeshafunguliwa.

Pia mashindano ya taifa na ile ya Olympic ya kufuzu ilifanywa kwenye maeneo ambayo huduma za vipimo kubaini ikiwa wanamichezo wanatumia dawa zilizopigwa marufuku hayakuwa rahisi kufikika.