EURO 2016

Ujerumani yavutwa shati, wakati Uingereza ikipata ushindi muhimu

Mshambuliaji wa timu ya Uingereza, Daniel Sturridge, akishangilia bao la ushindi aliloifungua timu yake dhidi ya wales, 16 June 2016
Mshambuliaji wa timu ya Uingereza, Daniel Sturridge, akishangilia bao la ushindi aliloifungua timu yake dhidi ya wales, 16 June 2016 REUTERS/Christian Hartmann Livepic

Goli lililofungwa kwenye dakika za lala salama na mshambuliaji, Daniel Sturridge, lilitosha kuipa ushindi muhimu timu ya taifa ya Uingereza, kwa kuwafunga mahasimu wao timu ya taifa ya Wales kwenye michuano ya kombe la Ulaya inayoendelea nchini Ufaransa.

Matangazo ya kibiashara

Makosa ya mlinda mlango wa Uingereza, Joe Hart, yalimruhusu mshambuliaji wa Wales, Gareth bale kuipatia bao la kuongoza timu yake, kutoka na mpira wa adhabu uliopigw anje kidogo ya eneo la 18.

Kocha mkuu wa timu ya Uingereza alijikuta yeye pamoja na wachezaji wakizomewa wakati wakielekea mapumziko, huku mashabiki tayari wakiwa na hofu kuhusu hatma ya timu yao ikiwa ingepotoza mchezo huo.

Hata hivyo, kipindi cha pili kocha Roy Hodgson aliwaingiza wachezaji Jarmie Vardy na Daniel Sturridge kuchukua nafasi ya Raheem Sterling na Harry Kane, mabadiliko ambayo ni wazi yalimuokoa dhidi ya aibu iliyokuwa impate.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Ireland Kaskazini wakipongezana baada ya kupata ushindi dhidi ya Ukraine.
Wachezaji wa timu ya taifa ya Ireland Kaskazini wakipongezana baada ya kupata ushindi dhidi ya Ukraine. REUTERS/Jason Cairnduff Livepic

Mabadiliko hayo yaliisaidia Uingereza, kwani katika dakika ya 56, mshambuliaji Jarmie Vardy aliipatia timu yake bao la kusawazisha, kabla ya dakika za lala salama, mchezaji Daniel Strurridge kuipatia timu yake bao la ushindi.

Kwa matokeo hayo, sasa Uingereza itakuwa inaongoza kundi B, ikiwa na alama 4, Wales wakifuatia wakiwa na alama 3 sawa na Slovakia huku Urusi yenyewe ikiwa na alama moja.

Uingereza inahitaji alama moja tu wakati itakapocheza na Slovakia ili kujikatia tiketi ya kutinga kwenye hatua ya 16 bora, huku Wales wao wakihitaji ushindi dhidi ya Urusi ikiwa wanataka kutinga hatua hiyo.

Katika mechi nyingine, timu ya Ireland Kaskazini imefanikiwa kupata ushindi wa kihistoria kwenye michuano ya mwaka huu ya kombe la Ulaya, baada ya kufanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ukraine.

Mchezaji wa Poland, Slawomir Peszko akiwania mpira na mchezaji wa Ujerumani Benedikt Howedes, wakati timu hizi zilipokutana, June 16, 2016
Mchezaji wa Poland, Slawomir Peszko akiwania mpira na mchezaji wa Ujerumani Benedikt Howedes, wakati timu hizi zilipokutana, June 16, 2016 Poland's Slawomir Peszko in action with Germany's Benedikt Howed

Beki wa klabu wa West Brom, Gareth McAuley aliunganisha vema pasi ya Oliver Norwood kuiandikia timu yake bao la kuongoza kabla ya mchezaji wa Niall McGinn kuiandikia timu yake bao la pili na la ushindi na kuipa timu yake ushindi muhimu katika kipindi cha miaka 34 toka imeshiriki mashindano hayo.

Mabingwa wa dunia mwaka 2014 timu ya taifa ya Ujerumani yenyewe ilijikuta ikilazimishwa sare ya bila kufungana na timu ya taifa ya Poland, kwenye mchezo uliokuwa wa upinzani mkubwa.

Kwa matokeo haya, yanamaanisha kuwa Ukraine inaondolewa rasmi kwenye hatua ya makundi, huku Ireland kaskazini ikijihakikishia angalau kumaliza kwenye nafasi ya tatu kutoka kundi C.