EURO 2016

Patashika nguo kuchanika kombe la Ulaya 2016, mechi za kundi C na D

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Poland, Adam Nawalka.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Poland, Adam Nawalka. REUTERS/UEFA/Handout

Michuano ya kombe la Ulaya 2016, inatarajiwa kuendeala kutimua vumbi Jumanne ya wiki hii, kwa mechi za kundi C na D kupingwa kwenye viwanja vinne tofauti, kutafuta timu ambazo zitakata tiketi ya kuingia kwenye hatua ya 16 bora.

Matangazo ya kibiashara

Majira ya saa moja kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki, timu ya taifa ya Ukraine itakuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Poland, mechi ya kundi C, ambayo itapigwa kwenye uwanja wa Vélodrome, mjini Marseille.

Ukraine inaingia kwenye mchezo huu ikiwa tayari imeshayaaga mashindano ya mwaka huu, na inashikilia mkia kwenye kundi C ikiwa haijapata alama yoyote, huku wapinzani wao timu ya Poland wenyewe wakiwa kwenye nafasi ya pili na alama 4.

Kocha wa kikosi cha Poland, Adam Nawałka, amekataa kuidharau timu ya Ukraine kutokana na timu hiyo kutofanya vizuri kwenye mechi zake za awali, ambapo amesema kuwa ataingia uwanjani kuhakikisha anashinda mchezo huo na pengine kumaliza kinara kwenye kundi lake.

Mchezaji wa Ujerumani akijaribu kuwatoka wachezaji wa Poland wakati timu zilipokutana.
Mchezaji wa Ujerumani akijaribu kuwatoka wachezaji wa Poland wakati timu zilipokutana. 路透社

Adam Nawałka, ameongeza kuwa Ukraine ni timu nzuri kwakuwa pia imetoa timu kadhaa ambazo zimeshiriki vizuri kwenye michuano ya klabu bingwa Ulaya na ile ya Europa ligi, na kwamba hawataibeza kwakuwa wanafahamu nao wataingia uwanjani wakiwa na lengo moja tu, la kuaga michuano ya mwaka huu kwa ushindi.

Kwa upande wake kocha mkuu wa Ukraine, Mykhailo Fomenko, amesema kuwa anafahamu timu yake haijawa na wakati mzuri sana kwenye mashindano ya mwaka huu, lakini hakusita kuwapongeza wachezaji wake kwa namna walivyoonesha kiwango licha ya kupoteza mechi zake zote mbili.

Olexandre Zinchenko kiungo kinda wa timu ya taifa Ukraine
Olexandre Zinchenko kiungo kinda wa timu ya taifa Ukraine REUTERS/Rafael Marchante

Mykhailo Fomenko, ameongeza kuwa timu yake itaingia uwanjani dhidi ya Poland, ikiwa na lengo moja tu la kusaka ushindi na wao kuondoka kwenye michuano ya mwaka huu wakiwa na angalau ushindi kibindoni, jambo ambalo amesema ameshawaambia wachezaji wake kuhakikisha wanafanikisha kupatikana kwa ushindi.

Kwenye mechi nyingine ya kundi C, Ireland ya Kaskazini yenyewe itakuwa inawakaribisha mabingwa wa dunia Ujerumani, kwenye mechi ambayo, timu zote mbili zinahitaji kupata ushindi ikiwa kila mmoja anataka kutinga kwenye hatua ya 16 bora.

Ireland ya Kaskazini inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na alama 3, huku Ujerumani yenyewe ikiingia kwenye mtanange huu ikiwa na alama 4, na leo itakuwa inahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kuongoza kundi lake wakati ikiingia kwenye hatua ya 16 bora.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Ireland Kaskazini wakipongezana baada ya kupata ushindi dhidi ya Ukraine.
Wachezaji wa timu ya taifa ya Ireland Kaskazini wakipongezana baada ya kupata ushindi dhidi ya Ukraine. REUTERS/Jason Cairnduff Livepic

Kocha mkuu wa Ireland Kaskazini, Michael O'Neill, amesema kuwa anafahamu mchezo wa leo dhidi ya Ujerumani ni mgumu, na kwamba kwao ni muhimu zaidi kushinda kwakuwa ushindi ama sare inaweza kuwavusha kwenye hatua ya 16 bora, lakini anachotarajia kutoka kwa wachezaji wake ni ushindi na sio vinginevyo.

O’Niell, anasema kuwa wanaingia kwenye mchezo huu wakifahamu umuhimu wa wao kushinda lakini nia ya Ujerumani ambayo nayo inasaka ushindi ili wavuke kwenye hatua ya 16 bora, kwahivyo kwa namna yoyote ile mchezo wao utakuwa mgumu.

Kwa upande wake kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Ujerumani, Thomas Schneider, amesema lengo kubwa la kikosi chake ni kuona wanamaliza wakiwa vinara wa kundi lao na si vinginevyo, kwa hivyo ushindi dhidi ya Ireland Kaskazini ni muhimu kuliko kawaida.

Ujerumani inaingia kwenye mchezo wa leo bila ya wachezaji wake muhimu, Boateng, Khedira na Özil ambao wanatumikia adhabu ya kadi za njano walizolimbikiza kwenye michezo iliyopita.

Mechi za kundi D pia zinatarajiwa kuendelea, ambapo timu ya taifa ya Croatia itakuwa na kibarua dhidi ya Uhispania kwenye mchezo ambao unatazamwa kwa ukaribu na wapenzi wa soka si tu barani Ulaya lakini duniani kwa ujumla.

Ante Coric, kiubgo wa timu ya taifa ya Croatia
Ante Coric, kiubgo wa timu ya taifa ya Croatia REUTERS/John Sibley

Uhispania inaingia kwenye mchezo huu, ikijua fika kuwa tayari imeshakata tiketi ya kucheza hatua ya mtoano ya michuano ya mwaka huu kwa kujikusanyia alama 6 kibindoni, huku wenzao Croatia wako kwenye nafasi ya pili wakiwa na alama 4, huku wakihitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya mtoano na pengine kumaliza wa kwanza kwenye kundi lao.

Kocha wa Croatia, Ante Čačić, anasema kuwa mchezo wao dhidi ya Uhispania ndio utakaoamua nani anamaliza kwenye nafasi ya kwanza kutoka kwenye kundi lao, na kuongeza kuwa ni muhimu kwa timu yake kuhakikisha inachomoza na ushindi wa kishinda kutengeneza mazingira mazuri zaidi.

Wachezaji wa timu ya taifa wakifanya mazoezi kabla ya kuanza kwa michuano ya Euro
Wachezaji wa timu ya taifa wakifanya mazoezi kabla ya kuanza kwa michuano ya Euro REUTERS/Javier Barbancho

Kwa upande wake kocha wa Uhispania, Vicente de Bosque, anasema suala la kuwapumzisha baadhi ya wachezaji au la, hajalipa kipaumbele kuelekea mchezo huu, kwakuwa anaamini wachezaji wengi wameshazoe mechi za michuano ya mwaka huu na pengine itakuwa vema zaidi ikiwa wataendelea kucheza kuliko kuwapumzisha, uamuzi ambao amesema anaufikiria na ataamua saa chache kabla ya mechi yenyewe.

Mechi nyingine kwenye kundi D, itazikutanisha timu ya taifa ya taifa ya Jamhuri ya Czech yenye alama 1 kwenye kundi lake, dhidi ya timu ambayo ni wazi imeshaaga mashindano ya mwaka huu, timu ya taifa ya Uturuki.

Wachezaji wa Jamhuri ya Czech wakiwa hawaamini baada ya kufungwa na Uhispania kwa bao 1-0, 13 June 2016
Wachezaji wa Jamhuri ya Czech wakiwa hawaamini baada ya kufungwa na Uhispania kwa bao 1-0, 13 June 2016 REUTERS/Albert Gea Livepic

Mchezo wa leo ni muhimu kwa Jamhuri ya Czech kuhakikisha inapata ushindi, ikiwa inataka kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kusonga mbele kuingia kwenye hatua ya mtoano, kitu ambacho wachezaji wa timu hiyo wanasema ndio ndoto yao.

Kocha mkuu wa Jamhuri ya Czech, Pavel Vrba, amesema kuwa kimtazamo na namna mambo yalivyo kwenye kundi lao, huenda wakahitaji kupata alama moja pekee ili kuwavusha kwenye hatua inayofuata, lakini akaongeza kuwa ni muhimu kwa timu yake kupata ushindi ikiwa inataka kusonga mbele.

Kwa upande wake kocha mkuu wa Uturuki, Fatih Terim, amesema kuwa timu yake iko kwenye kundi la kifo, na kwamba ili pengine kuweka angalau matumaini ya uwezekano wa wao kusonga mbele kwenye hatua ya mtoano, itabidi wafanye kazi ya ziada kuhakikisha wanachomoza na ushindi.