RIADHA

Kenya yasema iko tayari kuwapima wanariadha wake

Kipchoge Keino rais wa Kamati ya Michezo ya olimpiki nchini Kenya
Kipchoge Keino rais wa Kamati ya Michezo ya olimpiki nchini Kenya sportalnz

Kamati ya Michezo ya Olimpiki nchini Kenya, imekaribisha agizo la Kamati ya Kimataifa IOC kutaka wanariadha wake kupimwa kuelekea michezo ya Olimpiki itakayofanyika nchini Brazil mwezi Agosti.

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumanne, IOC ilisema mifumo nchini Kenya na Urusi kushindwa kubaini na kukabiliana na matumizi ya dawa za kuwaongezea nguvu wanamichezo, inakuwa vigumu kuwaamini wanariadha ikiwa hawatumii dawa hizo au la.

Tayari Shirika la Kimataifa linalopambana na dawa hizi WADA lilitangaza kuwa Kenya na Urusi zilikuwa zimeonesha kutotoa ushirikiano katika vita dhidi ya janga hili, hatua ambayo ilisababisha Kenya kupitisha sheria ambayo tayari imewasilishwa kwa uongozi wa Shirika hilo.

Mkuu wa michezo ya Olimpiki nchini Kenya Kipchoge Keino amesema tayari wanariadha zaidi ya 60 wakiwemo wachezaji wa mchezo wa raga tayari wameshafanyiwa uchunguzi huo na mwingine utafanyika kabla ya kuanza kwa michezo ya Olimpiki.

Miongoni mwa wanariadha ambao tayari wameshafanyiwa uchunguzi huo ni pamoja na wale watakaoshiriki katika mashindano ya duniani ya riadha kwa vijana wasiodizi miaka 20, yatakayofanyika mwezi Julai mjini Bydgoszcz, nchini Poland.